Raila ashtumu TSC kwa kudhoofisha KNUT

Muhtasari

 • Raila alisema tangu malumbano kati ya Knut na TSC yaanze idadi ya wanachama wa Knut imepungua kutoka 187,000 hadi 23,000.

  • Mapato ya muungano huo yalipungua kutoka Shilingi milioni 144 hadi shilingi milioni 15 pekee kila mwezi.

Aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga
Raila Odinga Aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga

Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ameshtumu Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) kwa madai ya kuua muungano wa kitaifa wa Walimu, KNUT.

Katika taarifa yenye maneno mazito, kinara huyo wa ODM alisema:

"Kupitia mfululizo wa vitendo vya kukusudia, TSC imelemaza na sasa iko katika harakati za kuua muungano wa Knut."

 

"Walimu huenda walitishwa na kunyamazishwa huku wakishuhudia kusambaratika kwa muungano waliyoujenga tangu mwaka 1957. Lakini hawafurahii," alisema Raila.

Tangu maridhiano na rais Uhuru Kenyatta, Raila amekuwa mpole kwa serikali, hatua ambayo wafuasi wake wanadai imeathiri umaarufu wake kabla ya 2022.

Katibu mkuu wa Knut Wilson Sossion na afisa mkuu mtendaji wa TSC Nancy Macharia
Katibu mkuu wa Knut Wilson Sossion na afisa mkuu mtendaji wa TSC Nancy Macharia

Siku ya Alhamisi, Raila alihoji sababu ya kuwepo kwa tofauti kubwa baina ya knut na TSC hali ambayo alisema imesambaratisha muungano wa knut ambao ulikuwa wa kuigwa na miungano mingine katika kutetea maslahi ya wafanyikazi nchini.

"Mzozo kati ya Tume ya TSC na KNUT unatishia kuua muungano ambao umekuwa wa kuigwa katika kutetea maslahi ya wafanyikazi," alisema.

Raila alisema kwamba tangu malumbano kati ya Knut na TSC yaanze mwaka 2018, idadi ya wanachama wa Knut imepungua kutoka 187,000 hadi 23,000.

Kulingana na maafisa wa Knut mapato ya muungano huo yalipungua kutoka Shilingi milioni 144 hadi shilingi milioni 15 pekee kila mwezi.

"Hali hii inaathiri shughuli za knut ambayo inahitaji angalau Shilingi milioni 80 kuwalipa wafanyikazi wake waliosambaa kote nchini," Raila alisema.

 

Raila aliilaumu TSC kwa kupuuza maagizo ya mahakama na mapendekezo ya bunge kuhusu suluhisho kwa suala hilo.