Mwilu asema madai dhidi yake hayamzuii kuwa kaimu jaji mkuu

Muhtasari

  • Mwilu alimwambia Jaji kwamba uadilifu wa jaji haupungui au kuisha wala haachi kutekeleza majukumu yake kwa sababu ya madai dhidi yake.

Naibu Jaji mkuu Philomena Mwilu
Naibu Jaji mkuu Philomena Mwilu

Madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka mbele ya Tume ya Huduma za Mahakama hayawezi kunizuia kuchukua nafasi ya kaimu Jaji Mkuu, Naibu jaji mkuu Philomena Mwilu ameambia korti.

Mwilu alimwambia Jaji Anthony Mrima kwamba uadilifu wa jaji haupungui au kuisha wala haachi kutekeleza majukumu yake kwa sababu ya madai dhidi yake.

Kupitia mawakili wake Nelson Havi na Julie Soweto, Mwilu alisema kesi yake haiwezi kuwa tofauti.

 

Naibu Jaji Mkuu alikuwa akijibu kesi iliyowasilishwa na mwanaharakati Okiya Omtatah kumzuia kuchukua kwa muda wadhifa wa jaji mkuu kutoka kwa David Maraga atakapostaafu mnamo Januari 12.

Omtatah anataka Mwilu asubiri hadi tume ya JSC itakapotoa uamuzi kuhusu madai ya ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi  dhidi yake.

Siku ya Jumatano, Mwilu aliambia korti kwamba kaimu jaji mkuu hateuliwi na JSC na kwamba tume hiyo haiwezi kufanya kazi ambayo haijapewa.

 JSC imeshirikishwa katika kesi hiyo lakini bado haijawasilisha kesi wala kujibu madai hayo.

"Sio kwa masilahi ya umma kwa wakenya kunyimwa huduma za jaji mkuu majukumu ambayo nastahili kutekeleza kama  kaimu jaji mkuu, sijafikia kiwango cha kusimamishwa au kuondolewa ofisini, ”alisema.

Katika kesi yake, Omtatah ameomba korti ifutiliye mbali barua ya Disemba 11, 2020  ya Maraga inayomteua Mwilu kuchukua wadhifa wa Jaji Mkuu kwa muda hadi nafasi hiyo ijazwe.

Mwanaharakati huyo alimwambia Jaji Mrima kuwa hakuna sheria  inayotoa muongozo wa kumteua Kaimu Jaji Mkuu. Kwa hivyo, ilani ya Maraga kwamba Mwilu achukuwe nafasi ya CJ ilikuwa kinyume na katiba.