Maraga aanza likizo ya kustaafu, malumbano kuhusu mrithi wake yaibuka

Muhtasari

• Jaji mkuu David Maraga aanza likizo yake ya kustaafu.

• Kuna njama kumzuia naibu jaji mkuu Philomena Mwilu kumrithi Maraga.

• Mwaharakati Okiya Omutata amewasilisha kesi dhidi ya Mwilu.

Jaji mkuu David Maraga. (Picha: HISANI )
Jaji mkuu David Maraga. (Picha: HISANI )

Jaji mkuu David Maraga siku ya Ijumaa alianza likizo yake ya kustaafu. Maraga ambaye atakumbukwa kwa kutekeleza maguezi mengi katika idara ya mahakama na kupunguza marudufu mrundiko wa kesi atastaafu rasmi mwezi Januari mwaka ujao.

Huku Maraga akiondoka ofisini malumbano ya kimya kimya lakini makali kuhusu udhibiti wa mahakama ya juu yameibuka katika idara hiyo.

Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu anatarajiwa kuchukuwa nafasi ya Maraga, kama kaimu jaji mkuu.

Lakini saa chache kabla ya Mwilu kuandika historia kama mwanamke wa kwanza nchini Kenya kushikilia nafasi ya jaji mkuu, mwanaharakati Okiya Omtatah amefika kortini akitaka mahakama imunzuie Mwilu kuchukuwa wadhifa huo.

Jaji Mkuu David Maraga akishauriana na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu na Jaji Smokin Wanjala wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais, Novemba 14, 2017. Picha: JACK OWUOR
Jaji Mkuu David Maraga akishauriana na Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu na Jaji Smokin Wanjala wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais, Novemba 14, 2017. Picha: JACK OWUOR

Omtatah anataka mahakama izuie tume ya Huduma kwa Mahakama kumteua Mwilu kuchukua nafasi katika ofisi hiyo yenye ushawishi hadi pale atakapoondolewa madai yote ya ufisadi dhidi yake. Mwilu amekanusha madai yote.

"Ni kwa masilahi ya umma na kwa masilahi ya haki kwamba naibu jaji mkuu aondolewe madai dhi yake au apatwe na hatia na JSC," Omtatah alisema kortini.

Imeibuka, hata hivyo, kwamba kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022, kuteuliwa kwa mrithi wa Maraga na kujaza nafasi ya Jackton Ojwang katika mahakama ya Juu kumezuia hali ya vuta ni kuvute baina ya wadau mbali mbali.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba uchaguzi wa rais wa 2022 huenda utafika katika mahakama ya juu kwa uamuzi wa mwisho.

Siku ya Alhamisi, Rais wa Chama cha Wanasheria wa Kenya Nelson Havi aliiambia Star kwamba "deep state" imeazimia kuhakikisha Mwilu hamrithi Maraga

"Deep State wameamua kuzuia naibu jaji mkuu kutwaa majukumu ya jaji mkuu katika kipindi cha mpito wakati wa likizo ya kustaafu ya Maraga," Havi alisema.