Kuidhinishwa kwa muswada wa BBI kunatenganisha kelele na ukweli - Kibicho

Muhtasari

•  Kibicho alisema matokeo ya 'Super Tuesday' yanaonyesha kwamba Wakenya wanaamini BBI kukuza utaifa na uzalendo.

Katibu wa kudumu wa mambo ya ndani Karanja Kibicho katika mahojiano ya Radio Jambo siku ya Jumatano, Februari 23, 2021.
Katibu wa kudumu wa mambo ya ndani Karanja Kibicho katika mahojiano ya Radio Jambo siku ya Jumatano, Februari 23, 2021.
Image: MINISTRY OF INTERIOR

Katibu wa kudumu wa mambo ya Ndani Karanja Kibicho ameyapongeza mabunge ya kaunti kwa uungaji mkono wao mkubwa kwa Muswada wa Mabadiliko ya sheria, 2020.

Hii ni baada ya Muswada kupita hitaji la angalau mabunge ya Kaunti 24 yanayohitajika ili kuendelea na hatua inayofuata.

Katika mahojiano na Radio Jambo Jumatano asubuhi, Kibicho alisema kwamba kupitia mchakato wa BBI, Wakenya wameweka wazi kuwa hawataki nchi iliyowekwa mateka na ghasia kila wakati wa uchaguzi.

"Uungwaji mkono na asilimia 90 ya mabunge ya kaunti ni jibu zuri kutofautisha kelele na ukweli. Inaonyesha Wakenya wameelewa na kuchagua njia ya upatanisho kulingana na nguzo za uwakilishi wa haki na ugawaji wa rasilimali, "Kibicho alisema.

Katibu huyo wa kudumu aliongeza kuwa matokeo ya 'Super Tuesday' yanaonyesha kwamba Wakenya wanaamini BBI kukuza utaifa na uzalendo.

Kibicho pia alisema kuwa BBI inalenga kutoa suluhisho la uhasama kati ya makabila na vikundi vya kisiasa.

Alisema, BBI itamaliza uhasama mkali na ushindani kati ya makabila na vikundi vya kisiasa.

Siku ya Jumanne, mabunge 23 ya kaunti yalipitisha Muswada huo kwa pamoja na kufikia sasa jumla ya mabunge 40 yameidhinisha muswada huo.  

Kuidhinishwa kwa muswada huo kulionekana kama ushindi Mkubwa kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga ambao wamekuwa mstari wa mbele kupigia debe mswada huo.

Kufikia Jumanne, Bunge la Kaunti ya Baringo lilikuwa la pekee kupinga Mswada huo.