NCIC yaelezea hofu kuhusu semi za uchochezi

Muhtasari

• Tume hiyo vile vile , imetoa tahadhari  kuhusu kuongezeka kwa ghasia za kikabila huko Marsabit, Turkana na Pokot Magharibi.

• Mwenyekiti Samuel Kobia alisema tume imeweka mikakati ya kuzuia na kuwakabili wanaoneza chuki uchaguzi wa 2022 unapokaribia.

Mwenyekiti wa NCIC Samuel Kobia
Mwenyekiti wa NCIC Samuel Kobia
Image: Maktaba

Tume ya Uiano (NCIC) imeibua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa visa vya matamshi ya chuki, uchochezi na kutovumiliana kisiasa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Tume hiyo vile vile , imetoa tahadhari  kuhusu kuongezeka kwa ghasia za kikabila huko Marsabit, Turkana na Pokot Magharibi.

Akiongea wakati alipofika mbele ya kamati ya seneti ya utangamano siku ya Jumatatu, mwenyekiti wa NCIC Samuel Kobia alisema kuwa wanasiasa wameanza kupiga ngoma za vita kwa kuchochea wafuasi wao katika kile alichosema kinaweza kusababisha vurugu nchini.

Hata hivyo, Kobia alituma onyo kwa wanasiasa, akisema wale ambao wamekusudia kueneza chuki na dharau za kikabila watakabiliwa na sheria kamili.

Alifichua kuwa tume imeweka mikakati ya kuzuia na kuwakabili wanaoneza chuki uchaguzi wa 2022 unapokaribia.

"Ubaguzi wa kikabila na unyanyasaji vimekuwa vyanzo vya mizozo huku matamshi ya chuki na dharau za kikabila vimekuwa vichocheo vya vurugu," Kobia alisema.

Mwenyekiti alifichua kwamba tume hiyo imetumia mfumo thabiti wa kugundua, kutoa taarifa na uchunguzi ili kuwakamata wachochezi.

NCIC, alisema, imeweka maafisa waliojitolea, wenye vifaa vya kurekodi ili kufuatilia mikutano ya hadhara na mikusanyiko ya kijamii ili kubaini matamshi ya chuki na ya kuchochea ghasia.

"Tume imeanzisha jukwaa la  kufuatilia mitandao ya kijamii kwa kubaini makosa chini ya Sheria ya NCIc," Kobia alisema.