Ruto aashiria kuhama Jubilee na kujiunga na UDA

Muhtasari

• Ruto alishtumu baadhi ya watu katika chama tawala kwa kutaka kukifanya Jubilee kuwa chama cha kikabila.

• Alisema kwamba ikiwa joto litazidi katika chama cha Jubilee watakikarabati chama cha UDA ili kiwe na sura ya kitaifa tayari kwa uchaguzi mkuu mwaka 2022.

Naibu rais William Ruto akiwa katika ziara za kukutana na wananchi
Naibu rais William Ruto akiwa katika ziara za kukutana na wananchi
Image: William Ruto Twitter

Naibu rais William Ruto ameashiria kukihama chama tawala cha Jubilee na kujiunga na chama kipya cha UDA.

Katika mahojiano kwenye kituo kimoja nchini siku ya Alhamisi, Ruto alishtumu baadhi ya watu katika chama tawala kwa kutaka kukifanya Jubilee kuwa chama cha kikabila.

Alisema ikiwa atasukumwa sana kwa ukuta katika Jubilee basi hatakuwa na budi ila kuhamia chama cha United Democratic Alliance (UDA) chama ambacho amehusishwa nacho kwa muda.

“ Kama utafika wakati hatuelewani tutajipanga na UDA kwa sababu ni chama tunajua na sera moja kwa sababu kimekuwa ndani ya Jubilee….UDA tutakifanya kiwe chama cha kitaifa. Kuna watu wanataka kufanya Jubilee chama cha kikabila na wakifanya hivo basi UDA tutakijenga kiwe chama cha kitaifa.” Ruto alisema.

Ruto alidai kwamba kuondolewa kwa seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen kutoka wadhifa wa kinara wa wengi katika Seneti na mwenzake wa Nakuru Susan Kihika kama kiranja wa wengi katika seneti kulichochewa kisiasa na baadhi ya watu katika chama cha Jubilee.

Kulingana na naibu rais makosa ya wawili hao na wengine wengi ambao walipokonywa nyadhifa zao bungeni yalikuwa kumuunga mkono.

Alisema kwamba ikiwa joto litazidi katika chama cha Jubilee watakikarabati chama cha UDA ili kiwe na sura ya kitaifa tayari kwa uchaguzi mkuu mwaka 2022.

 “leader of majority fukuzeni, pale Susan Kihika chief whip fukuza kwa sababu ni rafiki ya mtu fulani, haya ni mambo ambayo hayawezi kutusaidia…nguvu hizi zote kama tungekuwa tunazitumia kuendesha Big 4, tungekuwa saa hizi na nafasi ya kazi kwa vijana, tungekuwa tumetatua tatizo la chakula,” naibu rais alisema.

Naibu rais alitaja wito wa kufurushwa kwake kama naibu kinara wa Jubilee kama njama ya kuhujumu agenda ya maendeleo ya serikali kwa sababu za kibinafsi.

Alidai kwamba serikali ya Jubilee chini ya uongozi wa rais Uhuru Kenyatta ilitekeleza miradi mingi ya maendeleo katika kipindi cha kwanza cha uongozi wa Jubilee lakini mikakati yao imesambaratika katika muhula wa pili.

Alipepezea chini madai ya kutengwa katika baraza la mawaziri na katika mipango ya serikali, akisistiza kwamba anaangazia majukumu yake kama naibu rais wa Kenya.

“Mimi nimechaguliwa kama naibu wa rais wa Jamhuri ya Kenya, na katiba inanipatia nafasi ya kufanya kazi fulani, na hizo kazi mimi naendelea kuzifanya. Nani anahudhuria mkutano ni uamuzi wa rais, akiona pengine pale naibu wa rais hatakuwa na ya kuongezea, basi anaendesha vile yeye anavyopenda,” Ruto alisema.

Uhusiano kati ya rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto umeonekana kuzorota sana katika muhula wa pili wa uongozi wa Jubilee. Rais Kenyatta ameonekana kumpa majukumu mengi waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang’i hatua ambayo ilionekana kugadhabisha wandani wa naibu rais.

Naibu rais pia ameonekana kumkosoa kiongozi wake hadharani huku mara kadhaa akipinga baadhi ya sera za rais.

Licha ya kuwa naibu kinara wa Jubilee naibu rais amehusishwa sana na chama kipya cha UDA kinachoungwa mkono na wandani wake.