Magoha asema ratiba ya shule haitabadilishwa

Muhtasari

• Magoha siku ya Jumatatu alisema kwamba wazazi hawafai kuwa na wasi wasi kuhusu hatma ya wanafunzi ambao kwa sasa wanaendelea na likizo ya mwezi Aprili.

Waziri wa Elimu George Magoha

Waziri wa elimu George Magoha amewahakikishia wazazi kwamba ratiba ya shule itasalia kama ilivyokuwa imepangwa awali.

Magoha siku ya Jumatatu alisema kwamba wazazi hawafai kuwa na wasi wasi kuhusu hatma ya wanafunzi ambao kwa sasa wanaendelea na likizo ya mwezi Aprili.

Tangazo la rais Uhuru Kenyatta kuweka masharti makali mapya ya kudhibiti maambukizi ya Covid-19 liliibua hofu kuwa huenda ratiba ya shule ikaathirika kwa mara ya pili baada ya shule kufungwa kwa takriban mwaka mzima mwaka uliyopita.

Waziri Magoha alisema kwamba hajaona sababu ya kuitisha mkutano wa wadau katika sekta ya elimu kuangazia mabadiliko katika ratiba ya shule.

Alisema kulingana na takwimu za kitaifa idadi ya maambukizi ya Covid-19 imeanza kupungua.

Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kufungwa kwa taasisi zote za elimu mara moja na kulazimisha wanafunzi wote wa vyuo vikuu kurejea nyumbani kutokana na maambukizi ya Covid-19.

“Kwa vile inaonekana kwamba kiwango cha maambukizi kinaendelea kupungua, sioni umuhimu kuitisha wadau wa elimu kuangazia ratiba ya kalenda ya elimu upya. Kwa hivyo ratiba inasalia vile tulikubaliana awali mwakani, na kwa neema ya Mungu watoto wetu watarejea shuleni wakati waliostahili kufanya hivyo,’ Magoha alisema.

Katika masharti mapya ya kudhibiti maambukizi ya corona rais Uhuru Kenyatta pia alipiga marufuku kuingia na kutoka nje ya kaunti tano za Nairobi, Machakos, Kiambu, Kajiado na Nakuru.  Rais vile aliagiza kufungwa kwa mikahawa na maeneo yote ya burudani.

Katika tangazo hilo hata hivyo rais hakueleza ni muda upi masharti haya mapya yanafaa kuendelea kutekelezwa.