'Spiderman' akamatwa mjini Nairobi kuhusiana na wizi

Muhtasari

• Mshukiwa huyo ambaye alibandikwa jina "Spiderman 3" alitambuliwa kama Kennedy Otieno Oyier.

• Jambazi huyo  amekuwa akikwea kuta katika mitaa mbali mbali mjini  Nairobi na kuiba vifaa vya elektroniki, pesa na vito vya mapambo.

Mshukiwa baada ya kukamatwa
Mshukiwa baada ya kukamatwa

Jambazi ambaye amekuwa akikwea kuta katika mitaa mbali mbali mjini  Nairobi na kuiba vifaa vya elektroniki, pesa na vito vya mapambo amekamatwa.

Mshukiwa huyo ambaye alibandikwa jina "Spiderman 3" alitambuliwa kama Kennedy Otieno Oyier.

Kennedy ni ndugu wa mtuhumiwa mwingine - John Otieno Oyier- ambaye alikuwa amekamatwa mwezi Januari mwaka huu na kushtakiwa kortini kuhusu wizi na kuzuiliwa katika gereza la Viwandani, polisi walisema siku ya Jumatatu.

Kennedy alikamatwa siku Jumapili usiku katika operesheni kufuatia kuongezeka kwa visa vya wizi katika mitaa ya Kileleshwa, Parklands, Lavington, Muthangari na Westlands.

Amekuwa mafichoni baada ya kujua kwamba alikuwa kisakwa na maafisa wa polisi kwa siku kadhaa zilizopita Alikuwa akikimbia katika wiki zilizopita.

Alikuwa amebadilisha makazi yake baada ya kaka yake kukamatwa.

Kennedy aliwaambia polisi yeye na kaka yake walipata ustadi wa kukwea kuta kutoka kwa sinema ambayo walitazama mtandaoni.

Alisema wamefika kwenye makazi mengi katika maeneo hayo na kufanikiwa kuiba vitu vya thamani baada ya kuvunja nyumba kwa kutumia chuma na funguo.

Wanafanya hivyo wakikwepa mahali ambapo kuna taa au kamera.

Wanafanya hivyo mwishoni mwa wiki, asubuhi na mapema au wakati wa usiku wakati wenyeji hawako.

Baada ya kukamatwa, mshukiwa huyo aliwaongoza maafisa kwenda kwenye makazi yake huko Kawangware ambapo mabegi kadhaa ya laptop yalipatikana na magari mawili ambayo yalibururwa hadi Kituo cha Polisi cha Kilimani.

Polisi wanataka wale walioathiriwa kuzuru kituo hicho kufanikisha upelelezi.

Kukamatwa kulifuata msururu wa visa katika maeneo ambayo wakaazi walipoteza vitu vyao vya thamani na pesa.

Polisi wanaamini amekuwa akifanya kazi na walinzi wa nyumba ili kufanikisha wizi wake.

Afisa mkuu wa pilisi wa Nairobi Augustine Nthumbi alisema wanachunguza ili kubaini ikiwa mshukiwa anahusishwa na visa vingine vingi ambavyo vimeripotiwa katika maeneo mengine.

"Tunatafuta washukiwa zaidi ambao tunaamini walikuwa katika sakata hiyo," alisema.

Mshukiwa alikamatwa kwa kosa la wizi na anatarajiwa kortini leo Jumatatu.