Moses Kuria apigwa faini kwa kupuuza kanuni za Covid-19

Muhtasari

• Mbunge wa Gatundu Kusini Moses kuria na watu wengine 10 wamekiri mashtaka yanayohusiana na kupuuza kanuni za kudhibiti maambukizi ya Covid-19.

  • Mahakama hiyo iliwatoza faini ya shilingi 75,000 kila mmoja au kifungo cha miezi minane.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses kuria na watu wengine 10 wamekiri mashtaka yanayohusiana na kupuuza kanuni za kudhibiti maambukizi ya Covid-19 katika mahakama ya Kiambu.

 Mahakama hiyo iliwatoza faini ya shilingi 75,000 kila mmoja au kifungo cha miezi minane.

Watuhumiwa hao 11 walifikishwa mbele ya hakimu mkuu Stella Atambo.  Walikamatwa katika eneo la Karuri katika bustani ya Havilla cornerstone gardens mwendo wa saa tatu usiku wa Jumatatu na wengine 19.

 Hii ilikuwa baada ya polisi wa kituo cha Karuri kudokezewa kwamba kulikuwa na mkusanyiko wa kisiasa ambao ulikuwa kinyume na kanuni za kudhibiti maambukizi ya Covid-19.

Walikabiliwa na mashtaka matano ambayo ni pamoja na unywaji wa pombe, kukosa kutunza umbali wa mita moja unusu, kutovaa maski, kukusanyika bila idhini na kukiuka amri ya kutotoka nje.