Jaji Mkuu: Patricia Mbote ahojiwa kwa wadhifa wa Jaji Mkuu

Muhtasari

•Mbote aliambia JSC kwamba kwa sababu amekuwa muasisi wa taasisi mbali mbali na kuongoza zingine kote ulimwenguni anafaa kuwa jaji mkuu.

Profesa Patricia Mbote
Profesa Patricia Mbote

Profesa Patricia Mbote alikuwa mtu wa pili kupanda jukwaa kupigwa msasa kwa wadhifa wa jaji mkuu siku ya Jumanne baada ya Jaji Said Chitembwe kukunjua jamvi la mahojiano hayo siku ya Jumatatu.

 Mbote aliambia JSC kwamba kwa sababu amekuwa muasisi wa taasisi mbali mbali na kuongoza zingine kote ulimwenguni anafaa kuwa jaji mkuu.

Alianzisha kitivo cha mafunzo ya uanasheria katika chuo kikuu cha Strathmore na mashirika kama vile Women in law kama taasisi alizoanza tangu mwanzo.

 

Katika ulimwengu wa masomo, alisema, aliwahi kuwa mkuu wa kitivo katika Chuo Kikuu cha Nairobi kwa jumla ya miaka mitano akiongoza taasisi hiyo wakati mgumu

"Mimi sio kiongozi tu bali pia mjenzi wa taasisi," alisema wakati wa mahojiano ya nafasi ya jaji mkuu.

Ingawa uongozi hauna jinsia, Profesa alisema ana faida ya kuwa mwanamke kwa sababu ataleta zawadi ya kukuza.

Hata hivyo kama mwanamke katika uongozi alikumbana na changamoto kadhaa kama vile kutengwa au kudharauliwa kama mkuu wakati alikuwa na wenzake wa kiume wakiwa kwenye hafla mbali mbali.

"Niliwahi kwenda kwa mkutano na msajili ambaye ni mwanamume na kwa sababu sina mwili mkubwa, waandalizi walimkaribisha msajili kama mkuu wa kitivo  nikasema endelea," alisema.

Ikiwa atateuliwa kuwa jaji mkuu, Prof Mbote alisema, pia ataimarisha mahakama ya upeo kwa michango yake kulingana na kiwango chake cha elimu.

Alitoa mifano ya umuhimu wa mchango wa wasomi kwa korti wakati Mahakama ya upeo ilipoamua kukubali wasomi.

 

Ingawa hajafanya kazi kama wakili aliwahakikishia Wakenya kuwa yeye amefanya kazi na idara ya mahakama kama vile kuzalisha hati ya uboreshaji wa utendaji wa idara ya mahakama ambayo anasema imemsaidia kuwa kuelewa vyema taasisi hiyo.