Rais Samia aunda kamati ya kushughulikia janga la corona Tanzania

Muhtasari

• Rais Samia amesema kamati ikimaliza kazi yake atatoa taarifa rasmi.

•  ‘’Mtusaidie kusema na waumini kuhusu kujikinga, kinga ni bora kuliko tiba’’Alisema.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Image: HABARI MAELEZO TANZANIA

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameunda Kamati ya kumshauri kuhusu namna ya kushughulikia janga la corona nchini Tanzania.

Katika hotuba yake ya kuapisha Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu,alisema ataunda kamati ya kumshauri kuhusu hatua wanazoweza kuchukua kama nchi ili kujikinga na janga la corona.

''Nataka niwape taarifa kwamba tayari nilishaunda kamati hiyo na punde nitakaa nao pamoja na uongozi wa Wizara ya Afya na Wizara ya Fedha ili waone namna gani ya kushughulikia suala hilo''. alisema Rais Samia.

Lakini wakati kamati ikiendelea kufanya kazi, Rais Samia amewaomba viongozi wa dini kuwahimiza waumini kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na wataalamu wa afya.

‘’ Niwasihi mtumie kasi ile ile ya uelemishaji mwaka jana tulipotangaza kuwepo kwa ugonjwa huu, itumike sasa kwani mfumo wa maradhi haya ni ya kupanda na kushuka’’

‘’Mtusaidie kusema na waumini kuhusu kujikinga, kinga ni bora kuliko tiba’’Alisema.

Rais Samia amesema kamati ikimaliza kazi yake atatoa taarifa rasmi.