Ndoa ya Jubilee na UDA yayumba, Jubilee yataka talaka

Muhtasari

• Jubilee hata hivyo ilisema kwamba wanachama wa PDR ambao wanashikilianafasi za uongozi katika bunge wataendelea kuhudumu katika nafasi zao ingwa chama hicho kitasitisha shughuli zozote na PDR (UDA).

Katibu mkuu wa Jubilee
Katibu mkuu wa Jubilee

Dhoruba katika chama tawala cha Jubilee zaendelea kuyumbisha chombo huku chama hicho kikianzisha mchakato wa kukitaliki chama cha UDA chenye uhusiano wa karibu na naibu rais William Ruto. 

Jubilee kupitia kwa katibu mkuu wake Raphael Tuju kimeandikia msajili mkuu wa vyama vya kisiasa kikitaka kusitisha kabisa uhusiano wake na chama UDA awali kikijulikana kama PDR. 

Chama hicho katika barua kwa msajili wa vyama vya kisiasa kilisema kwamba kulingana na hali ya kisiasa kwa sasa nchini, imekuwa vigumu kuendelea na ushirikiano baina yake na chama cha UDA.

Tuju vile vile alisema kwamba maafisa wote wa chama cha PDR  ambao walitia saini makubaliano ya ushirikiano na Jubilee tayari washaondolewa na hata jina la chama likabadilishwa hadi UDA. 

Chama tawala pia kilishtumu UDA ambayo inaungwa mkono sana na wandani wa naibu rais William Ruto kwa kuwasilishwa wagombeaji katika chaguzi mbali mbali dhidi ya wagombeaji wa Jubilee kinyume na makubaliano kati ya vyama hivyo.

 “Maafisa wote wa PDR ambao walishiriki mazungumzo ya ushirikiano tayari wamebadilishwa na maafisa wapya wamekuwa wakidhihirisha uhasama kwa kuwasilisha wagombeaji katika maeneo nje ya eneo lililokubalika katika makubaliano ya ushirikiano,” Tuju alisema.

Jubilee ilisema pia kwamba kauli mbiu ya ‘Hustler nation’ inakwenda kinyume na sera za chama tawala ambacho kauli mbiu yake ni “Tuko Pamoja” inayolenga kuunganisha Wakenya na sio kuwagawanya kwa misingi ya kikabila au kwa misingi ya matabaka.

Tuju katika barua yake pia alishutumu baadhi ya wanachama wa UDA kwa kudhalilisha Jubilee na kufanya iwe vigumu kwa vyama hivyo kuendelea kufanya kazi pamoja.

"Kwa hivyo Chama kimeamua kusitisha ushirikiano wowote na PDR ambacho maafisa wake, alama na jina vimebadilika na sasa ni tofauti na PDR ambacho tulifanya kazi nacho  hapo awali," barua hiyo ilieleza.

Jubilee hata hivyo ilisema kwamba wanachama wa PDR ambao wanashikilianafasi za uongozi katika bunge wataendelea kuhudumu katika nafasi zao ingwa chama hicho kitasitisha shughuli zozote na PDR (UDA).

Naibu rais William Ruto katika mahojiano kwenye Citizen TV alisema kwamba ikiwa ataona hakaribishwi katika chama cha Jubilee basi hatakuwa na budi ila kuhamia chama cha UDA na kukijengwa ili kiwe na sura ya kitaifa.

Ruto alishtumu maafisa wa Jubilee kwa kusababisha malumbano katika chama na hata kukosoa vikali hatua ya katibu Raphael Tuju kumpiga marufuku dhidi ya kuzuru ofisi za chama tawala na ilhali yeye ndiye naibu kinara wa chama hicho.