Hakukuwa na utepetevu katika kifo cha Walibora kwa upande wa KNH

Muhtasari

• Uchunguzi wa kamati ya Seneti umeondolea lawama Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta dhidi ya madai ya utepetevu uliosababisha kifo cha mwandishi mashuhuri Prof Ken Walibora.

• Kamati hiyo hata hivyo, ilibaini kwamba Walibora alibaki hajulikani kwa siku tatu baada ya kifo chake kwa sababu ya kukosa hati za kitambulisho alipofikishwa hospitalini.

Marehemu Ken Walibora
Marehemu Ken Walibora
Image: MOSES MWANGI

Uchunguzi wa kamati ya Seneti umeondolea lawama Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta dhidi ya madai ya utepetevu uliosababisha kifo cha mwandishi mashuhuri Prof Ken Walibora mwezi Aprili mwaka jana.

Kamati ya Seneti ya Afya ilihitimisha uchunguzi wake baada ya miezi kadhaa, "Uzembe unaodaiwa hauwezi kuthibitishwa."

Walibora alitangazwa kuwa amefariki katika hosptali ya Kenyatta (KNH) alikokuwa amekimbizwa baada ya kugongwa na basi kwenye barabara ya Landhies Aprili 10, 2020.

Kulikuwa na madai kwamba Walibora alikuwa amelala akingojea msaada kwa saa 14 katika hospitali hiyo ya rufaa nchini, kwa kukosa kitanda cha ICU, na kusababisha kifo chake.

Lakini kamati hiyo, katika ripoti yake iliyowasilishwa kwa Seneti, ilisema Walibora alipokea hatua muhimu za dharura za kuokoa maisha wakati wa kulazwa.

"Alipata huduma za wagonjwa mahututi katika kitengo cha utunzaji muhimu cha idara ya Ajali na Dharura huko KNH," ripoti iliseme.

Kamati hiyo hata hivyo, ilibaini kwamba Walibora alibaki hajulikani kwa siku tatu baada ya kifo chake kwa sababu ya kukosa hati za kitambulisho alipofikishwa hospitalini.

Alisajiliwa hospitalini kama 'Mwanamume wa Kiafrika asiyejulikana'.

"Kama ilivyo kwa wahanga wa ajali na wenye bima ya kibinafsi, na ambao hawana hati za kitambulisho, ikiwa angetambulika angehamishiwa katika hospiali mbadala ya kibinafsi kwa matibabu zaidi," ilisema ripoti hiyo.

Iliongeza, "Ingawa madai ya utepetevu kwa upande wa KNH hayakuthibitishwa katika kifo cha Walibora, wahanga wengi wa ajali za barabarani na vurugu hufa kwa kukosa kupokea huduma za dharura kuokoa maisha yao."

Kwa hivyo, jopo lilisema kwamba mifumo inapaswa kuwekwa ili kuunganisha huduma za usajili wa raia na huduma za dharura za afya ili kuwezesha kutambua haraka wahanga wasiojulikana wa ajali.

Siku ya ajali, mwandishi anasemekana alitoka Lavington kwenda katikati mwa mji wa Nairobi. Kisha akatembea katikati mwa jiji akitafuta lori ya kusafirisha vifaa vyake kwenda nyumbani kwake eneo la Cherangany.

Na huko ndiko alikokutana na mauti.