Vugu vugu la mageuzi ya polisi lataka maafisa wahalifu kutemwa

Muhtasari

• Ufichuzi ulifunua jinsi maafisa wa polisi matukutu wanavyokuza uhalifu kwa kukodisha vifaa vyao vya kazi: bunduki, sare, vazi la kuzuia risasi, na pingu kwa wahalifu kwa chini ya shingi 1000.

Inspekta mkuu wa polisi Hillary Mutyambai
Inspekta mkuu wa polisi Hillary Mutyambai
Image: HISANI

Inspekta Jenerali wa Polisi ametakiwa kufanya ukaguzi huru na wa kina kuhusu mfumo wa uhifadhi, utoaji na uajibikiaji wa silaha na risasi kwa maafisa wa idara ya polisi.

Hii ni kufuatia makala maalum katika Citizen TV Aprili 18, 2021 "Guns Galore". Kulingana na makala hiyo maafisa wa idara za usalama nchini wamekuwa wakishirikiana wahalifu kwa kuwapa sare na silaha kutekeleza visa vya uhalifu.

 Ufichuzi ulifunua jinsi maafisa wa polisi matukutu wanavyokuza uhalifu kwa kukodisha vifaa vyao vya kazi: bunduki, sare, vazi la kuzuia risasi, na pingu kwa wahalifu kwa chini ya shingi 1000.

 Vuguvugu la kuleta mageuzi katika idara ya Polisi (PRWG-K) huku likishutumu vikali vitendo vya uhalifu ndani ya idara ya polisi, lilikiri kuwa bila shaka tabia za baadhi ya maafisa watovu zimekuwa kikwazo kwa usalama kote nchini.

Vuguvugu hilo kilibaini kuwa kulingana na ripoti za Kitengo cha Mambo ya Ndani ya idara ya polisi na ripoti ya Mamlaka huru ya shughuli za polisi IPOA kuna polisi ambao wamekuwa wakishiriki uhalifu.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, vuguvugu hilo lilitoa wito kwa Kamati ya Utawala na Usalama ya Kitaifa ya Bunge kufanya uchunguzi wa umma kuhusu suala la polisi kushiriki katika shughuli za uhalifu.

Pia wametoa wito kwa Kitengo cha Mambo ya Ndani kufanya uchunguzi wa kina na bila upendeleo wa madai ya utovu wa nidhamu wa polisi kwa nia ya kuwaondoa wahalifu.