Wakili wa Uhuru apigwa msasa kwa wadhifa wa Jaji Mkuu

Muhtasari

• Ngatia alisema kwamba kazi yake katika siku za mwanzo za taaluma yake ya uakili iliwezesha kumaliza mzozo wa mpaka kati ya Kenya na Sudan.

Wakili Fred Ngatia ajikwa mbele ya tume ya JSC
Wakili Fred Ngatia ajikwa mbele ya tume ya JSC
Image: CHARLENE MALWA

Wakili Fred Ngatia ambaye ana uzoefu wa kisheria wa miaka 41 siku ya Jumanne alijitosa mbele ya makamishna wa tume ya JSC kupigwa msasa kwa wadhifa wa Jaji mkuu.

Ngatia alisema kwamba kazi yake katika siku za mwanzo za taaluma yake ya uakili iliwezesha kumaliza mzozo wa mpaka kati ya Kenya na Sudan.

Anasema anafaa zaidi kuongoza idara ya mahakama nchini.

Anasema kazi yake ya utafiti ilisaidia Kenya kupata eneo lenye ukubwa wa mita 9680 mraba ambayo ni kubwa kuliko mkoa wa zamani wa Magharibi.

Mwaka wa 1914 mpaka kati ya Sudan na Kenya uliamriwa kama laini moja kwa moja.

Sehemu hizo za malisho huko Turkana hazikuwa zimefafanuliwa lakini uchunguzi katika miaka ya 1930 ulisema mpaka huo ulikuwa mstari uliowekwa.

Sudan kisha ikaja na kitu kinachoitwa Patron line. Lakini mwishowe utafiti wa Ngatia ulisaidia kusogeza mpaka kuipatia Kenya ushindi.

Ngatia pia alijipa sifa kwa kupatikana kwa ardhi ambapo uwanja wa michezo wa Kasarani umejengwa.

Image: CHARLENE MALWA

Wakili Ngatia hata hivyo alikiri kuwa analogi na kwamba yeye hupenda kukaa kwenye maktaba akisoma na sio kwa mitandao.

Ngatia alikiri kwamba yeye hayuko katika mitandao ya kijamii.

"Ninapendelea faraga ya kuwa kwenye maktaba kuliko kuwa kwenye mitandao ya kijamii,".

Ngatia alisema yeye ni miongoni mwa mawakili wachache ambao hawana kurasa za mitandao ya kijamii.

Hata hivyo alisema sio kwamba anadunisha mawakili wengi walio kwenye mitandao ya kijamii lakini hilo ni chaguo lake la kibinafsi.

Alikuwa akimjibu Profesa Mugenda ambaye alitaka kujua ni kwanini anasema hapendi mitandao ya kijamii na kulingana na wasifu wake anamiliki magari ya kifahari.