Amos Wako: Nilikuwa tayari kufa, azungumzia safari yake ya Corona

Muhtasari

• Ndani ya saa chache za kuthibitishwa kuwa na Covid-19, aliamini kwamba atakufa na kwa hivyo alianza kujiandaa kwa maisha ya baada ya mauti.

• Katika hospitali, aliwekwa kwenye oksijeni kila wakati, huku madaktari na wauguzi wakifuatilia hali yake kwa karibu. Maagizo yao yalimuogopesha, alisema.

• Walimshauri asiondoe mirija ya oksijeni. Ikiwa angepuuza maagizo hayo hata kwa dakika mbili, angekufa.

Seneta wa Busia Amos Wako
Seneta wa Busia Amos Wako
Image: EZEKIEL AMING'A

Mnamo Februari 17, seneta wa Busia Amos Wako alilazwa katika hospitali moja mjini Nairobi kwa wiki tatu chini ya uangalizi mkubwa baada ya kuambukizwa virusi vya Covid-19.

Hisia ya kuwa katika hali ya kukosa uwezo wa kujisadia, kutawaliwa, maumivu, na kujongea mauti uligeuza ulimwengu wake chini, ilibidi abadilishe malengo yake na cha muhimu kwake katika maisha - ilikuwa wakati wa kutafakari.

Wako, mwenye umri wa miaka 74, aliiambia KBC katika mahojiano ya kipekee ambayo yalipeperushwa hewani Jumapili usiku kwamba virusi havijui utajiri, nguvu na mafanikio.

 

Katika kipindi chote cha mahojiano ya dakika 45, Mwanasheria huyo Mkuu wa zamani aliyekuwa na ushawishi mkubwa alisema mara kwa mara: "Ni jambo la kutisha nisingemtakia mtu yeyote. Karibu nife."

Katika hospitali, aliwekwa kwenye oksijeni kila wakati, huku madaktari na wauguzi wakifuatilia hali yake kwa karibu. Maagizo yao yalimuogopesha, alisema.

Walimshauri asiondoe mirija ya oksijeni. Ikiwa angepuuza maagizo hayo hata kwa dakika mbili, angekufa.

"Wasiwasi wangu ulikuwa kwamba ikiwa nitalala na mirija ichomoke, na muuguzi haji kwa wakati, singeamka," Wako alisema.

Ndani ya saa chache za kuthibitishwa kuwa na Covid-19, aliamini kwamba atakufa na kwa hivyo alianza kujiandaa kwa maisha ya baada ya mauti. Alikuwa na vitabu vitatu vya kiroho — alivisoma zote.

"Kwa saa chache au zaidi, nilidhani 'huu ndio mwisho wangu.' Mwisho wangu umefika.Ndio maana ilibidi niende kiroho, kujiandaa kwa mahali ambapo ninaweza kujikuta ikiwa kila kitu kingine kimeshindwa.

"Sasa nilikuwa najiandaa kwa maisha ya baadae," Wako alisema.

 

Wako alisema vitabu hivyo vilipunguza mawazo yake nas kubaini mambo muhimu sana maishani. Alirekebisha vipaumbele vyake. Alikuwa tayari anatafakari vile matendo yake ya zamani yangechangia maisha katika maisha yake ya baada ya mauti.

"Kilicho muhimu ni [maswali kama] ikiwa ningefika kwenye ulimwengu unaofuata, nimefanya nini? Nini sijafanya? Na nimefanikiwa nini?" alisema.

"Nimemkosea nani? Huenda nisiwe na wakati wa kuomba msamaha na kurekebisha - niliomba kwa Mungu nipewe muda zaidi wa kufanya marekebisho hayo.

"Pia nilifikiria kuhusu wale ambao wanaweza kuwa walinikosea, ambao wengine wamekufa na sikutafuta kuafikiana nao."

Wako alisema upweke hospitalini ulimpa wakati mzuri wa kutathmini maisha yake "na nilikuwa tayari kwenda". Ilibadilisha mtazamo wake wa maisha.

"Baada ya kupitia na kuwa karibu na kifo, mtu yeyote ambaye amepitia ugonjwa huu, mtazamo wao hubadilika."

Alisema amebadilika, akiongeza kuwa haangalii tena mtazamo ule ule.

"Kuna maeneo kadhaa ambayo mitazamo yangu imebadilika. Vipaumbele vyangu vimebadilika," aliongeza.

Masaibu yake yalianza mnamo Februari 15 alipohudhuria mazishi ya waziri wa zamani Simeon Nyachae na baadaye mazishi ya aliyekuwa seneta wa Garissa Yusuf Haji siku moja.

Angehisi uchovu wa ajabu; alikuwa hata na ugumu kutembea kuelekea kwenye gari lake na alijitahidi kukumbuka majina ya watu anaowajua vizuri.

Alisema alikuwa akipata dalili za virusi kama kikohozi, matatizo ya kupumua na joto lakini akazipuuza kwa sababu alikuwa akitumia dawa za kuimarisha kinga kinga, tangawizi na mchanganyiko wa limao na dawa zingine zilizosemekana kuwa nzuri dhidi ya virusi.

"Nilitupilia mbali hisia hizo. Nilidhani kuwa hali yangu ya kisukari ndiyo iliyokuwa mbaya. Unaweza kuwa ugonjwa wowote isipokuwa Covid," alisema.

Alianza pia kuwa na ndoto za kuogofya, wakati mmoja, alisema, akiamka saa tisa au saa 4 hivi asubuhi na kumlalamikia mtoto wake kwa nini ilikuwa asubuhi na bado hakukuwa na jua.

"Hapo ndipo mwanangu aliposema ninahitaji kulazwa hospitalini haraka."

Kwa hiyo siku mbili baadaye, alikwenda katika hospitali moja jijini. Kwa mshangao wake, madaktari walimwambia hatarudi nyumbani — lazima alazwe hospitalini. Aliomba hata saa moja aruhusiwe kurudi nyumbani kwake kuchukua vitabu kadhaa vya ili awe na kitu cha kufanya katika kitanda chake cha hospitali.

Baada ya vuta ni kuvute wa muda mrefu, walikubaliana lakini kwa sharti kwamba wangemchukua katika ambulansi na kumrudisha haraka iwezekanavyo.

“Hapo ndipo mawazo yangu yalibadilika. Sikuweza kupewa hata saa moja kurudi nyumbani kwangu, kuchukuwa kile nilichotaka na kujisalimisha kwa hiari hospitalini, ”Wako alisema.

Wakati gari la wagonjwa lilipokuwa likiingia kwenye barabara zilizosongamana na trafiki na king’ora kilichokuwa kikilia, Wako alijiuliza ikiwa watu wanajua ni yeye aliyekuwa ndani. Akifuatana na wahudumu wa afya waliovaa mavazi meupe, alifika nyumbani kwake. Aliingia ndani, akachukua vitu vyake, na madaktari, na wakarejea hospitalini.

"Madaktari walisema ikiwa ningechukua siku mbili au tatu zaidi kabla ya kwenda kuangaliwa, ningekufa. Nilikosa kifo kwa tundu la sindano,” alisema.

"Nisingekuwa hapa leo. Ningekuwa mwanasheria mkuu wa zamani aliyewahi kuishi."

Wakati matibabu yakiendelea, madaktari walifikia uamuzi kwamba adungwe dawa za steroids ili kuimarisha uthabiti wa mapafu yake, ambayo yalikuwa karibu kuishiwa nguvu.

 Alisema hii ilifanya safari yake ya matibabu kuwa mbaya kwani ilizidisha hali yake ya kisukari.

Kiwango chake cha sukari kilipanda zaidi. Madaktari waliacha steroids na kuanza tena kushugulikia hali yake kisukari.