Raila alaani matumizi mabaya ya polisi Bonchari na Juja

Muhtasari

• Kinara wa upinzani aliwanyooshea kidole cha lawama maafisa wakuu wa serikali kwa kutumia nyadhifa zao kutumia vibaya mamlaka ya polisi.

• Raila alisema matukio hayo hayakustahili kwani 'mchakato wa uchaguzi ni fursa kwa wapiga kura kuelezea mapenzi yao kupitia kura hiyo.'

Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upunzani
Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upunzani
Image: MAKTABA

Kiongozi wa ODM Raila Odinga amelaani matumizi mabaya ya polisi kuwangaisha wapiga kura katika uchaguzi mdogo wa ubunge maeneo ya Bonchari na Juja.

Alisema matukio kama haya hayafai kuwepo.

Kinara huyo wa upinzani aliwanyooshea kidole cha lawama maafisa wakuu wa serikali kwa kutumia nyadhifa zao kutumia vibaya mamlaka ya polisi.

Raila aliwatahadharisha maafisa wa serikali kwa kugeuza uwanja wa uchaguzi kuwa "mwanya wa kujitafutia umaarufu kwa manufaa yao ya kibinafsi."

Alitaja matukio katika chaguzi ndogo kama "onyesho la kiburi la udhalilishaji wa sheria na maafisa wanaotaka kuonyesha kuwa wanafanya kazi."

Kiongozi huyo wa ODM aliwaonya maafisa hao dhidi ya kuchukua kwa urahisi amani ambayo imekuwepo nchini baada ya mwafaka baina yake na rais Uhuru Kenyatta, 2018.

"Ushirikiano wa amani haupaswi kuchukuliwa kwa urahisi na baadhi ya watu wahuni wanaotaka kutumia ‘handshake’ kama kisingizio cha kudhalilisha uhuru wetu uliopatikana kwa ugumu," Raila alisema.

Polisi walitwaa kituo cha kuhesabia kura cha Juja katika shule ya upili ya Mang’u Jumanne usiku, na kuwafukuza wanasiasa ambao walikuwa wakifuata shughuli ya kuhesabu kura.

IEBC iliripoti kuwa upigaji kura ulivurugwa na kundi la watu walioongozwa na gavana wa Kiambu James Nyoro, na kufanya mchakato huo usiweze kuendelea.

Matukio hayo yalisababisha polisi kuchukua jukumu la kulinda kituo cha hesabu na kurejesha utulivu.

Viongozi wa ODM walilalamika kuhusu unyanyasaji wa polisi katika uchaguzi wa Bonchari,  huku ripoti zikidai kuwa polisi walimkamata Mweka Hazina wa chama hicho Timothy Bosire (mbunge wa zamani wa Kitutu Masaba).

Kulikuwa pia na ripoti za uvamizi wa polisi katika makazi ya Gavana wa Kisii James Ongwae.

UDA ya naibu rais William Ruto pia alilalamikia vitisho vinavyolenga wagombea wake, maafisa, na mawakala.

Raila alisema matukio hayo hayakustahili kwani 'mchakato wa uchaguzi ni fursa kwa wapiga kura kuelezea mapenzi yao kupitia kura hiyo.'

"Vikosi vya usalama vipo kuwatumikia watu na sio masilahi ya wale wanaotaka kufanya majaribio ya kisiasa," kiongozi wa ODM alisema katika taarifa siku ya Jumatano.

Pavel Oimeke wa ODM - mkurugenzi mkuu wa zamani wa EPRA, alishinda uchaguzi wa Bonchari naye Francis Muraya wa UDA akishinda katika wadi ya Rurii.