ODM yatamba Bonchari huku Oimeke akishinda

Muhtasari

• Oimeke, ambaye alikuwa ametimuliwa wadhifa wa mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta na kawi, alipata kura 8,049  kuibuka mshindi.

Mbunge mteule wa Bonchari Pavel Oimeke akipokea cheti cha kushinda uchaguzi wa eneo bunge la Bonchari.
Mbunge mteule wa Bonchari Pavel Oimeke akipokea cheti cha kushinda uchaguzi wa eneo bunge la Bonchari.
Image: MAGATI OBEBO

Mgombea wa ODM Pavel Oimeke ndiye mbunge mteule wa eneo bunge la Bonchari.

Oimeke, ambaye alikuwa ametimuliwa wadhifa wa mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mafuta na kawi, alipata kura 8,049  kuibuka mshindi.

Zebedeo Opore wa Chama cha Jubilee alipata kura 7,279 kuchukua nafasi ya pili huku Teresa Bitutu wa UDA akimaliza wa tatu kwa kura 6,964.

Jumanne, Oimeke alidai kupitia kile alitaja kama "vitisho na unyanyasaji wa wafuasi wake wengi kupata ushindi mtamu".

Hiki ni kiti cha ubunge cha kwanza kwa chama cha ODM baada ya kupoteza viti vyote mwaka 2018.

Maafisa wa chama cha ODM wakiongozwa na Gavana James Ongwae na katibu mkuu Edwin Sifuna wakisubiri kutangzwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Bonchari.
Maafisa wa chama cha ODM wakiongozwa na Gavana James Ongwae na katibu mkuu Edwin Sifuna wakisubiri kutangzwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Bonchari.
Image: MAGATI OBEBO

Hakuna mbunge mwingine isipokuwa Gavana James Ongwae, Seneta Sam Ongeri na Mwakilishi wa Wanawake waliochaguliwa kwa tikiti ya ODM katika kaunti ya Kisii.

Maafisa wa ODM walidai kuhangaishwa na polisi katika uchaguzi huo huku ikidaiwa kuwa baadhi ya viongozi walikuwa wamezingirwa na polisi.

Gavana James Ongwae alidai kuwa zaidi ya polisi 50 walikuwa wamevamia boma lake usiku kabla ya uchaguzi kufanyika hatua iliopelekea gavana huyo kuandaa mkutano na wanahabari akikashifu waziri wa usalama Fred Matiang’I kwa kupanga uvamizi huo.

Ongwae alisema kwamba maafisa hao walivuruga chakula chao cha jioni alipokuwa na wageni wake maafisa wengine wa ODM katika boma lake eneo la Maili Mbili.

Marehemu mbunge wa Oroo Oyioka alikuwa ameshinda kiti hicho kwa tiketi ya chama cha People's Democratic Party, kilinachohusishwa na aliyekuwa mbunge wa South Mugirango Omingo Magara ambaye kwa sasa ni mshirika wa chama cha UDA.

Aliongoza kampeni za UDA na kumpigia debe mjane wa marehemu Oroo, Teresa Bitutu.