Israel na Palestina zasitisha mapigano

Muhtasari

• Israeli imeukubali mpango wa Misri wa kusitisha mapigano mabaya zaidi kuwahi kutokea tangu mwaka 2014, na imekubali bila masharti yoyote.

• Nchi kadhaa zimehusika katika majadiliano hayo ya muda mrefu ikiwemo Misri, ambayo ni mshirika wa karibu wa pande zote mbili kwa sasa.

• Pande zote mbili zimekuwa zikikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka jamii ya kimataifa kumaliza uhasama.

Mashariki ya kati
Mashariki ya kati
Image: GETTY IMAGES

Mashambulizi baina ya Israel na Palestina yamesimamishwa, baada ya siku 11 za ghasia kati ya pande hizo mbili.

Israeli imeukubali mpango wa Misri wa kusitisha mapigano mabaya zaidi kuwahi kutokea tangu mwaka 2014, na imekubali bila masharti yoyote.

Misri sasa inatarajiwa kutuma wajumbe nchini Israeli na Ukanda wa Gaza katika siku chache zijazo kwa lengo la kuumaliza kabisa mgogoro huu.

Maafisa wa Hamas wanasema huenda makubaliano ya sasa yakawa na nguvu iwapo tu Israel itaacha kutumia nguvu katika masuala ambayo yanahitaji diplomasia, huku Israel ikisema Hamas inahitaji kushauriana vyema na mamlaka ya Palestina ili kunusuru machafuko mengine.

Nchi kadhaa zimehusika katika majadiliano hayo ya muda mrefu ikiwemo Misri, ambayo ni mshirika wa karibu wa pande zote mbili kwa sasa.

Rais wa Marekani Joe Biden amesema mazungumzo ya siku 11 yamesaidia kufikia mafanikio hayo.

Rais wa Marekani Joe Biden aliitaka Israel kuwanusuru raia wasio na hatia
Rais wa Marekani Joe Biden aliitaka Israel kuwanusuru raia wasio na hatia
Image: GETTY IMAGES

Baada ya habari hiyo kutangazwa, kulikuwa na mashambulio zaidi ya anga ya Israeli huko Gaza na makombora yalirushwa kuelekea Israeli. Wakati huo huo, uwanja mkuu wa ndege wa nchi hiyo, Ben Gurion, ulifungwa kwa muda mfupi kutokana na hofu ya usalama.

Hali ya mambo ilivyo kutokana na uharibifu wa majengo
Hali ya mambo ilivyo kutokana na uharibifu wa majengo
Image: MOD

Inaarifiwa kuwa muda mfupi baada ya kutangazwa kusitishwa kwa mapigano, mamia ya watu wameanza kurejea katika makazi yao, licha ya miundombinu na nyumba zao kuharibiwa vibaya.

Hamas imeadhibiwa, na Wapalestina wa Gaza wameteseka sana. Wachambuzi wa siasa za Mashariki ya kati wanasema ili kuepuka mgogoro mwingine, ni vyema mahitaji ya pande hizi mbili yakafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

Rais Biden alisema nini ?

Akiongea katika Ikulu ya White House, Rais Joe Biden alisema alimpongeza Bw Netanyahu kupitia simu baada ya kutangazwa makubaliano ya kusitisha mapigano.

"Marekani inaunga mkono kikamilifu haki ya Israeli ya kujilinda dhidi ya mashambulio ya roketi ya kiholela kutoka Hamas na vikundi vingine vya kigaidi vya Gaza ambavyo vimeua watu wasio na hatia nchini Israeli," Bwana Biden alisema.

Alisema waziri mkuu wa Israeli alitambua kama yeye mfumo wa ulinzi unaojulikana kama Iron Dome, "ambao mataifa yetu yalitengeneza pamoja na ambao umeokoa maisha ya raia wa Israeli - wote Waarabu na Wayahudi".

Bwana Biden pia alimsifu Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi kwa kufanikisha kusitisha mapigano, kabla hayajasababisha maafa ya watu wengi.

"Natuma pole zangu za dhati kwa familia zote, Israeli na Palestina, ambao wamepoteza wapendwa wao na kuwatakia afueni ya haraka kabisa waliojeruhiwa," alisema.

Image: REUTERS

Rais alisema Marekani "inaendelea kujitolea kufanya kazi na Umoja wa Mataifa" katika kutoa msaada wa kibinadamu kwa Gaza na katika juhudi za ujenzi wa eneo hilo. Aliongeza kuwa hii itafanywa "kwa ushirikiano kamili na Mamlaka ya Palestina, sio Hamas".

Rais Sisi alisema alikuwa amepokea simu ya Bwana Biden na "furaha kabisa", na kuongeza kuwa "walibadilishana maono kuhusu jinsi ya kutafuta suluhisho ya kudumu kwa mzozo wa Gaza.

Nini kilipeleka mapigano kusistishwa?

Pande zote mbili zimekuwa zikikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka jamii ya kimataifa kumaliza uhasama.

Siku ya Jumatano, Rais wa Marekani Joe Biden alimwambia Bw Netanyahu "kwamba alitarajia kushuka kwa kiwango kikubwa kwa mapigano'.

Misri, Qatar na UN vimekuwa na jukumu la kuongoza mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Israeli na Hamas, ambayo inatawala Gaza.

Rais Sisi aliamuru makundi ya jumbe mbili za usalama kwenda Israeli na maeneo yaliyokaliwa ya Palestina kufanya kazi ili kufanikisha usitishaji wa vita, kulingana na Televisheni ya serikali ya Misri.