Prince Harry: 'Nilikunywa pombe kupindukia kuficha uchungu wa kifo cha mamangu'

Muhtasari

• Mtawala wa Sussex mwanamfalme Harry amesema alikuwa akinywa pombe yenye thamani ya wiki moja kwa siku kujaribu kukabiliana na huzuni ya kifo cha mama yake.

• Diana, Princess wa Wales, alikufa katika ajali ya gari wakati akifuatwa na wapiga picha huko Paris mnamo Agosti 1997.

Image: HARPO PRODUCTIONS - JOE PUGLIESE

Mtawala wa Sussex mwanamfalme Harry amesema alikuwa akinywa pombe yenye thamani ya wiki moja kwa siku kujaribu kukabiliana na huzuni ya kifo cha mama yake.

Prince Harry pia alikuwa tayari kutumia dawa za kulevya "kupunguza hisia alizokuwa nazo za simanzi' zaidi ya muongo mmoja baada ya kifo cha mamake Princess Diana

Harry alikuwa akiongea na mtagazaji maarufu wa televisheni Marekani Oprah Winfrey katika kipindi kipya cha kupeperushwa mtandaoni kuhusu afya ya akili.

Alizungumza pia juu ya wasiwasi na mashambulio ya hofu aliyokuwa nayo kama mmoja wa watendaji wakuu wa kifalme na aliyopitia wakati wa mazishi ya mama yake.

Diana, Princess wa Wales, alikufa katika ajali ya gari wakati akifuatwa na wapiga picha huko Paris mnamo Agosti 1997.

Akiongea na Oprah katika kipindi cha Televisheni cha Apple The Me You Can not See, Harry alielezea kuwa na umri wa miaka 28 hadi 32 kama "wakati mbaya katika maisha yangu", ambapo alikuwa na mshtuko wa hofu na wasiwasi mkubwa.

"Nilitatizika sana kiakili," alisema.

"Kila wakati ninapovaa suti na kufunga tai ... lazima nifanye jukumu hili , na kwenda, 'sawa, sura ya kazi ,' angalia kwenye kioo na kusema, 'twende'. Kabla hata sijaondoka nyumbani nilikuwa nikimimina jasho. Nilikuwa katika hali ya kupigana au kukimbia. "

Image: PA MEDIA

Aliongeza: "Nilikuwa tayari kunywa, nilikuwa tayari kutumia dawa za kulevya, nilikuwa tayari kujaribu kufanya vitu ambavyo vilinifanya nisihisi kama vile nilikuwa ninajisikia."

Alisema angekunywa pombe yenye thamani ya wiki moja Ijumaa au Jumamosi usiku, "sio kwa sababu nilikuwa nikifurahiya lakini kwa sababu nilikuwa najaribu kuficha kitu".

Prince Harry alitembea nyuma ya jeneza la mama yake kwenye mazishi yake, pamoja na kaka yake, baba yake, mjomba na babu yake.

"Kwangu mimi kitu ninachokumbuka zaidi ni sauti ya kwato za farasi zinazopita ..." alisema.

"Ilikuwa kama nilikuwa nje ya mwili wangu na nikitembea tu nikifanya kile kilichotarajiwa kutoka kwangu. Kuonyesha sehemu ndogo sana ya hisia ambazo kila mtu alikuwa akionyesha: huyu alikuwa mama yangu - haujawahi kukutana naye."

Harry mwenyeumri wa miaka 36, amefanya kampeni ya majadiliano juu ya afya ya akili kuwa ya kawaida, na akaanza kuzungumza kwa undani juu ya maisha yake kibinafsi hivi karibuni.

Mnamo Machi, yeye na mkewe Meghan walihojiwa na Oprah juu ya maisha yao katika familia ya kifalme, na athari zake kwa afya yao ya akili.

Na kwenye jarida la podcast wiki iliyopita, Prince Harry alisema alikuwa ameamua "kuvunja mzunguko wa maumivu" ya malezi yake wakati wa kuwalea watoto wake mwenyewe, na akafichua kwamba alikuwa amekwenda kwa matibabu.

Ameongeza kwamba wakati wa kufurahisha zaidi maishani mwake ni miaka yake 10 katika Jeshi, kwani hakukuwa na "matibabu maalum" kwake.

Aliondoka Jeshi akiwa na umri wa miaka 30, na alikutana na mkewe wa baadaye Meghan mwaka mmoja baadaye.

Harry alisema wanafamilia wake hapo awali walimwambia " Endelea kufanya kama maigizo tu na maisha yako yatakuwa rahisi".

"Lakini nina mengi ya mamangu ndani yangu," alisema. "Ninahisi kana kwamba niko nje ya mfumo - lakini bado nimekwama hapo. Njia pekee ya kujikomboa na kujitokeza ni kusema ukweli."

Kipindi hicho cha muendelezo kitawafanya Prince Harry, Oprah, Lady Gaga, Glenn Close na wengine wakielezea hadithi zao juu ya afya ya akili na ustawi.

Klitangazwa kwa mara ya kwanza mnamo Aprili 2019, karibu mwaka mmoja kabla ya Harry na Meghan kutangaza kuwa watajiondoa kutoka majukumu yao ya kifalme mnamo Januari 2020.