Raila, Kalonzo, Mudavadi waanzisha matumaini ya kufufua NASA

Muhtasari

• Raila alisema ni muhimu kwa viongozi kuweka kando asili zao za kikabila na kuungana kwa manufaa ya taifa la Kenya.

• Musalia alirejelea umuhimu wa viongozi wa Nasa kuaminiana ili kupata suluhisho kwa shida zinazowakumba Wakenya.

• Kalonzo alitoa wito kwa wenzake kuendelea kujenga madaraja yaliyovunjika.

Viongozi wa Nasa Raila Odinga, Musalia Mudavadi na Kalonzo Musyoka wakati wa maombi ya wafu ya aliyekuwa mbunge wa Gem Jakoyo Midiwo katika kanisa la Citam Valley Road, Nairobi Alhamisi, Juni 24, 2021 Picha: RAILA ODINGA PRESS TEAM
Viongozi wa Nasa Raila Odinga, Musalia Mudavadi na Kalonzo Musyoka wakati wa maombi ya wafu ya aliyekuwa mbunge wa Gem Jakoyo Midiwo katika kanisa la Citam Valley Road, Nairobi Alhamisi, Juni 24, 2021 Picha: RAILA ODINGA PRESS TEAM

TAARIFA YA MOSES ODHIAMBO 

Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga siku ya Alhamisi alitoa wito kwa viongozi wa Nasa kuungana tena kwa Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Akizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu mustakabali wa Nasa, Raila alisema vinara wanne wa Nasa Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Moses Wetang'ula na yeye mwenyewe wanahitaji kushirikiana ili kupeleka taifa la Kenya mbele.

Alikuwa akiongea wakati wa ibada ya wafu ya aliyekuwa mbunge wa Gem Jakoyo Midiwo aliyefariki wiki iliyopita. Ibada hiyo ilifanyika katika kanisa la Citam Valley Road jijini Nairobi. Musalia na Kalonzo walikuwepo.

Raila alisema ni muhimu kwa viongozi kuweka kando asili zao za kikabila na kuungana kwa manufaa ya taifa la Kenya.

"Roho ya Jakoyo inapaswa kufanya kazi kutuunganisha kwenda mbele," Raila alisema.

Chama chake cha ODM tayari kiko katika mazungumzo ya muungano na Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta.

Raila alitoa salamu za rambirambi za rais, akisema kwamba Uhuru hakuweza kuhudhuria maombi kwani alikuwa katika uzinduzi wa mashindano ya magari ya Safari Rally, mashindando ambayo yamerejea nchini baada ya miaka 19.

Aliwaomba Wakenya kuiga mfano wa Midiwo, akimtaja marehemu kama "Mkenya wa kweli ambaye alikuwa na maono wazi kuhusu vile Kenya inapaswa kuwa."

 “Midiwo angejielezea kwa hisia kali. Hakukubali kurudishwa nyuma. Hii iko katika jeni zetu. Unaweza kufuatilia tabia hii kwa wazazi wetu na babu na nyanya, ”Raila alisema.

Mazungumzo kati ya ODM na Jubilee ya Rais Uhuru Kenyatta yalikuwa yamezua wasiwasi kwamba muungano wa Nasa ambao tayari umekuwa ukiyumba yumba huenda ungeangamia kabisa.

Musalia, Kalonzo, na Wetangula siku ya Jumanne walifanya mkutano wa saa mbili jijini Nairobi kujadili mustakabali wao wa kisiasa.

Hotuba za Raila, Musalia na Kalonzo kwenye maombi ya Jakoyo zilionesha juhudi za pamoja za upinzani kusalia pamoja.

Musalia alirejelea umuhimu wa viongozi wa Nasa kuaminiana ili kupata suluhisho kwa shida zinazowakumba Wakenya.

"Tunapoendelea mbele, tufanye kazi pamoja, tujenge madaraja na kuunga mkono kila kitu tunachofanya kwa uaminifu na nina hakika suluhisho bora litapatikana kwa Wakenya," kiongozi huyo wa ANC alisema.

Alisema Kenya ni ya raia wote kwa hivyo viongozi wote wana jukumu la kulinda masilahi ya nchi.

“Lazima sote tuilinde; kutafuta kuwa na utawala bora, haki, uchumi ambao unafanya kazi kwa wote. Haya ndiyo mambo ambayo naamini Jakoyo aliyathamini, ”alisema.

Alisema ni busara kwa Wakenya kupata mafunzo kutoka kwa maisha na nyakati za Jokoyo.

"Tutafakari juu ya wakati ambao tulikuwa naye na nina hakika tutapata mafunzo kutoka kwake," Musalia alisema.

Jakoyo alisifiwa kwa kuwa hakuwa na mipaka katika urafiki.

Kalonzo aliahidi kwamba viongozi wa Nasa watajitahidi kufanya kazi pamoja. Alitoa wito kwa wenzake kuendelea kujenga madaraja yaliyovunjika.

Makamu huyo wa rais wa zamani alisema wana matumaini Mahakama ya Rufaa itatoa uamuzi wa busara kuhusu kesi ya mchakato wa BBI. Kesi hiyo itasikilizwa kuanzia Jumanne wiki ijayo.

"Tusubiri matokeo ya mchakato huo mbele ya Mahakama ya Rufaa. Tutegemee kuwa haki itatawala na mchakato wa mageuzi kwa faida ya nchi hii utaendelea. Nadhani haya ndio malengo ya juu zaidi, "Kalonzo alisema.

Viongozi kadhaa ambao walikuwepo waliwahimiza vigogo hao wa wa Nasa kufanya kazi pamoja ili kuafikia ahadi ya kuwapeleka wakenya katika mjini wa ‘Kanaani’.

Mbunge wa Makadara George Aladwa alianzisha mjadala katika hotuba yake.

"Ninasihi Kalonzo na Musalia kwamba ikiwa utamchukua ndugu yako kuoa na kugundua kuwa msichana amekwenda nje ya nchi kusoma, na msichana anarudi, lazima urudi na umchukue ili kuhakikisha kuwa msichana ameolewa," Mbunge wa Gem Elisha Odhiambo alisema.

Seneta wa Siaya James Orengo alisema, "Nataka kusihi kwamba huu ni wakati wa kuleta nchi pamoja. Hakutakuwa na wakati mwingine. ”

"Ikiwa Kenya haitajumuishwa pamoja wakati huu na kuanza pamoja kama nchi moja chini ya Mungu, itakuwa vigumu sana kuifanya hili siku nyingine. Jakoyo, akiwa ametuleta pamoja leo, roho yake itatuongoza kuungana, "Orengo aliongeza.

"Tuna viongozi wetu hapa - Raila, Kalonzo, na Musalia. Tuko mikononi mwenu. Fanyeni kitu," mwenyekiti wa ODM John Mbadi alisema.

Mbunge wa Gatanga Joseph Nduati alitoa wito kwa wakuu wa Nasa kuungana.

"Raila, Mudavadi, na Kalonzo, tunawaomba mkae pamoja na mtupe kiongozi ambaye atasimamia nchi," Nduati alisema.

(Imetafsiriwa na kuhaririwa na Davis Ojiambo)