MCGAKATO WA BBI

Majaji 7 wateuliwa kusikiza kesi dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu kupuuzilia mbali BBI

Jaji Musinga atasimamia kesi hiyo ambayo inatarajiwa kuanza kusikizwa Jumanne wiki ijayo

Muhtasari

•Kesi hiyo inatarajiwa kusikizwa kwa siku nne kuanzia Jumanne hadi Ijumaa, Julai 2. Baada ya hapo majaji hao watakutana na kuandika ripoti kuhusiana na maamuzi ya kesi.

•Mahakama kuu ilikosoa kuhusika kwa rais kwenye mchakato wa BBI na kutaja hiyo kama sababu moja ya kuutupilia mbali miongoni mwa makosa mengine yaliyotajwa.

RAIS WA MAHAKAMA YA KUKATA RUFAA DANIEL MUSINGA
RAIS WA MAHAKAMA YA KUKATA RUFAA DANIEL MUSINGA
Image: MAKTABA

Rais wa mahakama ya kukata rufaa, Daniel Musinga ameteua jopo la majaji saba ambao watasikiza kesi ya BBI.

Jaji Musinga atasimamia kesi hiyo ambayo inatarajiwa kuanza kusikizwa Jumanne wiki ijayo na kushirikiana na majaji wengine sita ambao ni jaji Roselyn Nambuye, Hannah Okwengu, Fatuma Sichale, Gatembu Kairu, Patrick Kiage na Francis Tuiyott waki.

Kesi hiyo inatarajiwa kusikizwa kwa siku nne kuanzia Jumanne hadi Ijumaa, Julai 2. Baada ya hapo majaji hao watakutana na kuandika ripoti kuhusiana na maamuzi ya kesi.

Kabla ya kusikiza kesi hiyo, jopo la majaji watatu litasikiza ombi la mwanasheria mkuu, Kihara Kariuki la kutaka ombi la wakili Charles Kanjama dhidi ya BBI kufutiliwa mbali. Kesi hiyo itasikizwa Jumatatu .

Rais Uhuru Kenyatta, kinara wa ODM Raila Odinga, mwanasheria mkuu na kamati ya BBI wote walikosoa uamuzi wa mahakama kuu kufupilia mbali mchakato wa BBI. 

Kupitia mawakili wao, wote hao waliwasilisha ombi la kupinduliwa kwa uamuzi huo katika mahakama ya kukata rufaa.

Mahakama kuu ilikosoa kuhusika kwa rais kwenye mchakato wa BBI na kutaja hiyo kama sababu moja ya kuutupilia mbali miongoni mwa makosa mengine yaliyotajwa.

Rais na Odinga wameendelea kuhakikishia wafuasi imani yao kuwa uamuzi wa mahakama kuu utatupiliwa mbali na 'reggea itachezwa tena'