SIASA ZA BBI

"BBI itahakikisha ujumuishaji na usawa" Rais aendelea kupigia debe BBI

Rais aliashiria matumaini yake kuwa BBI itafanikisha ujumuishaji na ugavi sawa wa rasilimali kote nchini.

Muhtasari

•Rais Kenyatta alisema kuwa kufanya kazi pamoja na viongozi wengine wa mirengo yote ya kisiasa kumemuwezesha kufanikisha miradi mingi zaidi kwenye muhula wake wa pili mamlakani kwani aliweza kuangazia maendeleo zaidi badala ya siasa.

•Amewaonya viongozi dhidi ya siasa mingi zinazopelekea kusahaulika kwa maendeleo huku akisema kuwa malumbano ya siasa na maslahi ya kibinafsi ya wanasiasa yanavuta nchi nyuma.

Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta
Image: Maktaba

Rais Uhuru Kenyatta ameendelea kupigia debe mchakato wa BBI licha ya mahakama kuu nchini kuupuuzilia mbali mwezi moja uliopita.

Akizungumza katika ikulu wakati alikuwa amekaribisha viongozi kutoka Ukambani siku ya Jumatatu, rais alisisitiza kuwa nia kuu ya mchakato wa BBI ni kuleta nchi pamoja na kujumuisha umoja wa taifa.

Rais aliashiria  matumaini yake kuwa BBI itafanikisha ujumuishaji na ugavi sawa wa rasilimali kote nchini.

BBI itahakikisha ujumuishaji na usawa. Itawafanya Wakenya kuhisi wamehusishwa” Rais Kenyatta alisema.

Alikuwa amekaribisha baadhi ya viongozi kutoka eneo la Ukambani wakiwemo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Gavana Charity Ngilu(Kitui) na Gavana Alfred Mutua(Machakos).

Rais amewasihi viongozi wote nchini kuungana na kufanya kazi pamoja ili kutimiza lengo la kuwa taifa la mapato ya kati kufikia mwaka wa 2030.

Amewaonya viongozi dhidi ya siasa mingi zinazopelekea kusahaulika kwa maendeleo huku akisema kuwa malumbano ya siasa na maslahi ya kibinafsi ya wanasiasa yanavuta nchi nyuma.

“Badala ya kujihusisha na siasa zisizoisha, tufanye kazi pamoja. Tunapofanya hilo, tutaweza kuwa taifa la mapato ya kati kufikia mwaka wa 2030” Rais alisema.

Rais Kenyatta alisema kuwa kufanya kazi pamoja na viongozi wengine wa mirengo yote ya kisiasa kumemuwezesha kufanikisha miradi mingi zaidi kwenye muhula wake wa pili mamlakani kwani aliweza kuangazia maendeleo zaidi badala ya siasa.

Kwa kufanya kazi pamoja na wenzangu, nimeweza kuangazia zaidi ajenda za maendeleo badala ya ajenda za kisiasa” Rais alisema.

Kalonzo alimshukuru rais kwa miradi ya maendeleo ambayo imetekelezwa Ukambani na serikali ya kitaifa akitoa mfano wa kufufuliwa kwa tume ya nyama nchini(KMC)

Ngilu na Mutua walithibitisha uungaji mkono wa agenda nne kuu za rais Kenyatta.