"Nilifulia watu nguo" Sakaja azungumzia alivyoweza kujikimu katika chuo kikuu

Sakaja alikiri kuwa angepata zaidi ya sSh6000 kila siku kutoka kwa biashara zake, jambo ambalo lilimuwezesha kunua gari na kupata nyumba akiwa chuo kikuu

Muhtasari

“Nikiwa katika chuo kikuu ilibidi nimejitafutia karo kwani familia yetu haikuwa na pesa sana. Kutokana na hayo, nilianzisha biashara tofauti. Nilikuwa na saluni, kinyozi, duka la dobi na nilipikia watu” Sakaja alisema

Johnson Sakaja
Johnson Sakaja
Image: Hisani

Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja ameeleza namna alivyoweza kutimiza ndoto yake ya kununua gari aina ya Mercedes Benz akiwa bado mwanafunzi wa chuo kikuu cha Nairobi.

Akizungumza kuhusu maisha yake kwenye kipindi cha Churchill Show, Sakaja ameeleza jinsi alivyojitokosa kwenye biashara aina tofauti ili kuweza kulipa karo na kukimu mahitaji yake.

“Nikiwa katika chuo kikuu ilibidi nimejitafutia karo kwani familia yetu haikuwa na pesa sana. Kutokana na hayo, nilianzisha biashara tofauti. Nilikuwa na saluni, kinyozi, duka la dobi na nilipikia watu” Sakaja alieleza Churchill.

Mwanasiasa huyo alikiri kuwa angepata  zaidi ya shilingi elfu sita kila siku  kutokana na biashara zake, jambo ambalo lilimuwezesha kunua gari akiwa katika mwaka wake wa nne pale chuo kikuu.

Sakaja alieleza kuwa aliweza kununua gari aina ya mercedes kwa Sh500,000 kutoka kwa Seneta wa Bungoma Moses Wetangula.

Gari hilo sikujua lilimilikiwa na Seneta Wetangula, nilikuja kugundua baadae. Wetangula alikuja kujua gari ambalo alikuwa anaona katika hoteli ya Serena ni yangu. Aliniambia kuwa angejua ni mimi nanunua angeniuzia bei nusu” Sakaja alisema.

Kando na gari hilo, Sakaja alikiri kuwa aliweza kuwa na nyumba yake pande za Yaya Center.

Seneta Sakaja pia alieleza kuwa alijitosa kwenye siasa za chuo kikuu akiwa mwaka wa pili na kuweza kupanda ngazi hadi kuwa rais wa muungano wa wanafunzi wa UON.

Siasa zile zilimfungulia njia hadi kuweza kumsaidia hadi kuwa seneta wa jiji la Nairobi.