Rais wa Haiti auawa katika shambulizi kwenye makazi yake

Muhtasari

• Mke wa Rais aliripotiwa pia kujeruhiwa katika shambulio hilo.

• Kulikuwa na maandamano yaliyoenea katika mji mkuu na miji mingine mapema mwaka huu, kwani watu walimtaka ajiuzulu.

Image: REUTERS

Rais wa Haiti Jovenel Moise ameuawa katika shambulio dhidi ya makazi yake mjini Port-au-Prince - amesema kaimu Waziri mkuu Claude Joseph

Bwana Joseph alisema makazi ya rais huko Port-au-Prince yalishambuliwa na watu wasiojulikana waliojihami kwa silaha saa 01:00 saa za eneo hilo (05:00 GMT).

Mke wa Rais aliripotiwa pia kujeruhiwa katika shambulio hilo.

Bwana Joseph alisema kuwa "hatua zote zilichukuliwa ili kuhakikisha kuendelea kwa serikali".

Image: GETTY IMAGES

Jovenel Moïse, 53, alikuwa madarakani tangu Februari 2017, baada ya mtangulizi wake, Michel Martelly kung'atuka mamlakani.

Wakati wa Bw Moïse ofisini ulikuwa mgumu wakati alipokabiliwa na tuhuma za ufisadi na alikabiliwa na mawimbi ya maandamano ya mara kwa mara ya kupinga serikali

Mwaka wa 2019 wakati wa mojawapo ya maandamano kama hayo rais huyo alisema 'Hatondoka nchini kwasababu ya shinikizo kutoka kwa magenge yaliyojihami na walanguzi wa dawa za kulevya'

Kulikuwa na maandamano yaliyoenea katika mji mkuu na miji mingine mapema mwaka huu, kwani watu walimtaka ajiuzulu.

Upinzani nchini humo ulisema kwamba kipindi cha miaka mitano cha Bw Moïse kilipaswa kumalizika tarehe 7 Februari 2021, miaka mitano hadi siku hiyo tangu Bw Martelly aondoke madarakani.

Bwana Moïse, hata hivyo, alisisitiza alikuwa na mwaka mmoja zaidi wa kutumikia kwani hakuingia madarakani hadi 7 Februari 2017.

Kucheleweshwa kwa mwaka mzima kulisababishwa na madai ya udanganyifu katika uchaguzi ambao mwishowe ulisababisha matokeo ya uchaguzi wa 2015 kufutiliwa mbali na kura mpya kufanywa ambapo Bw Moïse alitangazwa mshindi .

Image: REUTERS

Misukosuko ya muda mrefu, udikteta na majanga ya asili yameiacha Haiti kama moja ya mataifa masikini kabisa katika eneo la Amerika.

Tetemo la ardhi mwaka wa 2010 liliua zaidi ya watu 200,000 na kusababisha uharibifu mkubwa kwa miundombinu na uchumi.

Kikosi cha kulinda amani cha UN kilitumwa mnamo 2004 kusaidia kuleta utulivu nchini, na kiliondoka tu mnamo 2017.