Msaidizi wa Raila Odinga, Philip Etale ashambuliwa tena na COVID 19 baada ya miezi minne

Etale ametoa ombi kupumzika kutoka kwa mitandao ya kijamii hadi wakati atapata afueni.

Muhtasari

•Etale amesema kuwa kuanzia siku ya Jumatatu wiki iliyopita mwili wake umekuwa ukiashiria dalili zisizoeleweka na amekuwa akikohoa, kuumwa na kichwa na mapua yake kufungika ila mwanzoni alidhani kuwa ni homa tu ya kawaida.

•Mwezi wa Machi mwaka huu Etale alikuwa ameugua tena maradhi  hayo.

Image: FACEBOOK//PHILIP ETALE

Mkurugenzi wa mawasiliano katika chama cha ODM Philip Etale ametangaza kuathiriwa na maradhi  ya COVID 19 kwa mara ya pili.

Etale amesema kuwa kuanzia siku ya Jumatatu wiki iliyopita mwili wake umekuwa ukiashiria dalili zisizoeleweka na amekuwa akikohoa, kuumwa na kichwa na mapua yake kufungika ila mwanzoni alidhani kuwa ni homa tu ya kawaida.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook,  Etale amesema kuwa alitembelea hospitali ya Aghakhan baada ya hali yake kuzorota ambapo  alipimwa na kupatikana kuwa na virusi vya Korona.

"Marafiki wangu wapendwa, wimbi hili ni mbaya. Nilipoteza hisia ya harufu na hamu ya kula. Mwili unaniuma vibaya. Kichwa kinauma sana na mwili umechoka. Kiuno chauma hadi siwezi amka kutembea. Usiku wangu umesheheniwa na uchungu na sipati usingizi" Etale alisema.

Msaidizi huyo wa aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga ametoa ombi kupumzika kutoka kwa mitandao ya kijamii hadi wakati atapata afueni.

"Ninachowaomba ni maombi yenu. Asanteni na Mungu awabariki nyote" Etale alimalizia kwa kusema.

Mwezi wa Machi mwaka huu Etale alikuwa ameugua tena maradhi  hayo.