Siasa za mlima Kenya: Karua, Kuria na Kiunjuri kuandaa kongamano

Muhtasari

• Watatu hao walisema watawasiliana na vyama vyote vya kisiasa katika eneo hilo kuungana nao ili kufanikisha mipango yao.

• Karua alisema pia watawasiliana na wataalamu, vijana, viongozi wa dini, na viongozi wa biashara kusaidia kuendeleza azimio hilo.

Mbunge wa Gatundu kusini Moses Kuria, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na kiongozi wa chama cha TSP Mwangi Kiunjuri wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Nairobi, Agosti 12.2021
Mbunge wa Gatundu kusini Moses Kuria, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na kiongozi wa chama cha TSP Mwangi Kiunjuri wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Nairobi, Agosti 12.2021
Image: EZEKIEL AMING'A

Viongozi watatu wa Mlima Kenya wamezindua mikakati kuandaa kongamano la kuleta pamoja viongozi wa eneo hilo ili kupanga mustakabali wa kisiasa wa Mlima Kenya kabla ya uchaguzi wa 2022.

Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, mwenzake wa TSP Mwangi Kiunjuri na Moses Kuria wa Chama Cha Kazi walialika vyama vyenye nia moja kujiunga nao.

Watatu hao siku ya Alhamisi walisema watawasiliana na vyama vyote vya kisiasa katika eneo hilo kuungana nao ili kufanikisha mipango yao.

Walitangaza kwamba mkutano utafanyika mjini Limuru katika miezi mitatu ijayo ili kupata mwelekeo kuhusu mrithi wa rais wa Rais Uhuru Kenyatta.

Katika ushirikiano wao, wanasiasa hao walisema wamejitolea kufanya kazi pamoja katika maswala yanayoathiri Mlima Kenya na taifa "bila kujali mirengo yao ya kisiasa."

"Tunajitolea pia kufikia viongozi wengine wenye nia kama hii ili kupanua kongamano na kuimarisha umoja wetu wa kusudi," walisema katika taarifa iliyosomwa na Karua.

Alisema pia watawasiliana na wataalamu, vijana, viongozi wa dini, na viongozi wa biashara kusaidia kuendeleza azimio hilo.

"Katika miezi mitatu ijayo, mpango huo utafika kilele katika mkutano wa tatu wa Limuru ambapo tutafanya maazimio ya jinsi ya kufanya mambo yetu," Karua alisema.

Walisema kuwa sio kila mtu ambaye atajiunga nao atakuwa na msimamo sawa wa kisiasa, lakini kuna maswala mengi  ambayo yanaathiri eneo zima.

"Hili ni jukwaa lisilofafanua muungano wa kesho - linaweza kuishia kuwa hilo, lakini ni umoja wa kusudi kujadili maswala yanayoathiri mkoa wetu na taifa," Karua aliongeza.

Alisema mkutano ujao "utafafanua baadhi ya maswala ambayo yanavutia wote" lakini alikuwa mwepesi kusema kuwa vyama vya kibinafsi havitavunjwa.

"Lazima tulinde demokrasia yetu ya vyama vingi kwa kujenga vyama vyetu vya kisiasa na sio kuua vyama vingi ambavyo vilituchukua muda mrefu kufikia."