Sio kiki! Wanamuziki Nadia Mukami na Arrow Boy wadhihirisha wazi kuwa wanachumbiana

Malkia huyo wa muziki amesema kuwa walifanya maamuzi ya kujitokeza kwa kuwa haikuwa rahisi tena kwao kuendelea kujificha hadharani ilhali wanachumbiana kwa ufiche.

Muhtasari

•Siku chache zilizopita picha ya wawili hao wakibusu iliIbua gumzo kubwa mitandaoni huku wengi wakikadiria kuwa wasanii hao wanachumbiana.

•Nadia amepuuzilia madai ya kiki na kusema kuwa amehitimu umri ambapo anataka kuanza kutengeneza familia pamoja na mpenzi wake.

Image: INSTAGRAM//NADIA MUKAMI

Wanamuziki mashuhuri nchini Nadia Mukami na Arrow Boy wameweka wazi kuwa ni kweli wanachumbiana.

Kupitia video ya moja kwa moja kwenye mtandao wa Instagram ambayo walirekodi usiku wa Jumatano, wawili hao walitangaza kuwa wakati wao kujitokeza hadharani ulikuwa umewadia.

Siku chache zilizopita picha ya wawili hao wakibusu iliIbua gumzo kubwa mitandaoni huku wengi wakikadiria kuwa wasanii hao wanachumbiana.

Hata hivyo kunao baadhi ya mashabiki ambao walidai kuwa picha hiyo ambayo nyota hao wawili wa muziki wa kisasa walipakia kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii ilikuwa kiki tu. Baadhi ya wanamitandao walidai kuwa wawili hao walikuwa wakitafuta kiki kwani walikuwa na mpango wa kushirikiana kutoa wimbo.

Hata hivyo, Nadia amepuuzilia madai ya kiki na kusema kuwa amehitimu umri ambapo anataka kuanza kutengeneza familia pamoja na mpenzi wake.

" Sio kiki! naona watu hawaamini kwani kwa muda.. Hata mimi nimeanza kuzeeka, nahitimu miaka 25 mwaka huu. Inafikia wakati fulani ambapo unataka tu kufurahia maisha pamoja na mtu na unataka kujenga maisha ya usoni na mtu. Watu hawaamini, ni sawa. Hatuwezi badiliha dhana za mtu kutuhusu" Nadia alisema.

Malkia huyo wa muziki amesema kuwa walifanya maamuzi ya kujitokeza kwa kuwa haikuwa rahisi tena kwao kuendelea kujificha hadharani ilhali wanachumbiana kwa ufiche.

"Ilifikia wakati tukaona ni heri tujitokeze. Mambo yalianza kuwa magumu. Tungeenda kwa mikutano tunajifanya hatujuani ilhali tumetoka kulala pamoja .. tumekuwa kwa nyumba usiku uliokuwa umepita" Nadia aliendelea kusema.

Takriban miaka miwili iliyopita wapenzi hao wawili walishirikiana kutoa kibao 'Radio Love' ambacho kilivuma sana kote Afrika Mashariki.

Wimbo huo wa mapenzi ndio ulikuwa chanzo cha uvumi kuwa huenda wanachumbiana.