'Ondoa kafyu!' Mbunge Moses Kuria amwambia rais Kenyatta kufuatia kifo cha ndugu wawili Embu

Kulingana na Kuria, marehemu walikuwa wanajaribu kutafuta pato kubwa kutoka kwa biashara yao ya kuuza nyama ya nguruwe na ndio sababu wakachelewa kufunga.

Muhtasari

•Benson Njiru (22) na Emmanuel Mutura (19) ambao walikuwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Kabarak na chuo cha mafunzo ya kiteknolojia cha Don Bosco mtawalia wanadaiwa kukamatwa na polisi kutoka kituo cha polisi cha Manyatta mida ya usiku wa Agosti 1  kisha mili yao kupatikana katika mochari ya Embu siku mbili baadaye.

•Hafla ya kuwakumbuka ndugu Njiru na Mutura imepangwa kufanyika jioni ya leo (Alhamisi) nyumbani kwao katika kijiji cha Kithangari kaunti ya Embu.

Image: HISANI

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria amemwagiza rais Kenyatta kutupilia mbali amri ya kutotoka nje kama njia  ya kuonyesha mshikamano katika juhudi za kutafuta haki ya ndugu wawili waliofariki katika hali tatanishi Jumapili wiki iliyopita.

Benson Njiru (22) na Emmanuel Mutura (19) ambao walikuwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Kabarak na chuo cha mafunzo ya kiteknolojia cha Don Bosco mtawalia wanadaiwa kukamatwa na polisi kutoka kituo cha polisi cha Manyatta mida ya usiku wa Agosti 1  kisha mili yao kupatikana katika mochari ya Embu siku mbili baadaye.

Familia ya wawili hao ilisema kuwa walifahamishwa kuwa maafisa kutoka Manyatta walikamata ndugu hao wawili katika soko ya Kianjokoma walikokuwa wanauza nyama ya nguruwe.

Alipokuwa anaonyesha ushirikiano wake kwenye mtandao wa Facebook leo asubuhi (Agosti 12), Kuria alidai kuwa ndugu hao waliuliwa na maafisa wa polisi walipokuwa wanafanya kazi.

Kulingana na Kuria, marehemu walikuwa wanajaribu kutafuta pato kubwa kutoka kwa biashara yao ya kuuza nyama ya nguruwe na ndio sababu wakachelewa kufunga.

"Rais Uhuru Kenyatta. Ili kuonyesha mshikamanano na #KianjokomaBrothers, tunakuagiza kuondoa kafyu mara moja. Walikuwa wanajaribu tu kutafuta faida kubwa kutoka kwa biashara yao ya kuuza nyama. Waliuliwa na wakatili wako wanaovaa nguo za bluu wakiwa kazini yao. Kazi yao ya kuuza nyama ya nguruwe ni muhimu pia. Maliza kafyu sasa!" Kuria alisema.

Hafla ya kuwakumbuka  Njiru na Mutura imepangwa kufanyika jioni ya leo (Alhamisi) nyumbani kwao katika kijiji cha Kithangari kaunti ya Embu.

Wakenya ambao wana nia ya kuhudhuria hafla hiyo wametakiwa kubeba mchumaa kama ishara ya kuonyesha upendo kwa marehemu.

Image: HISANI

Maelfu ya Wakenya mitandaoni wameendelea kujumuika mitandaoni wakidai haki kutendeka kuhusiana na kifo cha ndugu hao wawili.

Chini ya alama ya reli #JusticeForKianjokomaBrothers kwenye mtandao wa Twitter, Wakenya wameendelea kushinikiza maafisa wa DCI kufanya upelelezi kuhusiana na tukio hilo kwa dharura na hatua kali kuchukuliwa dhidi ya wahusika