Mwanafunzi wa kidacho cha kwanza awasili shuleni bila kitu

Mwalimu mkuu wa shule ya Kanyawanga Jacob Mbogo na mwanafunzi John Otieno Odhiambo
Mwalimu mkuu wa shule ya Kanyawanga Jacob Mbogo na mwanafunzi John Otieno Odhiambo
Image: MANUEL ODENY

NA MANUEL ODENY 

Mwanafunzi mmoja siku ya Jumanne Agosti 24 aliwasili katika shule Shule ya Upili ya Kanyawanga katika kaunti ya Migori bila kitu chochote kujiunga na kidato cha kwanza.

Kulingana na mwanafunzi huyo juhudi za wazazi wake kumtafutia karo na bidhaa zingine za matumizi zilikua zimegonga mwamba.

John Otieno Odhiambo alisema aliuza ndizi alizopanda akiwa mwanafunzi katika

Shule ya Msingi ya Ng'ong'a ili kupata Shilingi 100 alizotumia kama nauli kutoka Awendo kwenda shuleni.

"Niliamka saa kumi na mbili asubuhi na kutembea hadi mjini Awendo, ambapo nilipanda gari hadi mjini Rongo na kutembea kwenda shule, nilitaka tu kwenda shule na kusoma kwasababu marafiki wangu wote katika kijiji walikuwa wamejiunga na kidato cha kwanza," Odhiambo alisema.

Odhiambo alisema alipata alama 337, na akasema alitamani kuwa daktari wa neva katika siku zijazo.

"Nilipata barua ya kujiunga na Shule ya Kanyawanga ambayo imekuwa shule yangu ya ndoto, kwa muda mrefu niliamua kutembea kwenda shule baada ya wazazi wangu kumaliza njia zote za kunilipia karo ya shule," Odhiambo alisema.

Alisema wazazi wake hufanya kazi za vibarua, "na njia zote za kupata karo ziligonga mwamba kabisa. Nataka tu kuwa shuleni na kusoma, ndio tu. ”

Odhiambo alisema alikuwa amefikia matumaini ya mwisho ya kwenda shule na aliamua tu kutembea baada ya kusikiliza redio kwamba waziri wa elimu George Magoha alitaka kuhakikisha wanafunzi wote wanakwenda shuleNI.

 "Aliingia shuleni kwa miguu na alikuwa amebeba tu matokeo yake, barua ya kujiunga na kidato cha kwanza na vitambulisho vya wazazi wake. Alikuwa na nguo zake za nyumbani na akasema alitaka kuruhusiwa kusoma, "mkuu wa shule hiyo Jacob Mbogo alisema.

Mboga alisema mnamo Agosti 6, baba ya mtoto huyo alikwenda shuleni na kuomba kuongezwa muda hadi Agosti 13 kwa kuwa shule hiyo haina ada au pesa ya kununua sare na mahitaji mengine ya kimsingi.

"Baada ya Agosti 13 tulijaribu kumtafuta kijana huyo kupitia shule yake ya msingi na utawala wa mkoa na hatukumpata, tumemuona tu shuleni leo," Mbogo alisema.

Alisema kutoka Jumanne, mvulana aliruhusiwa kulala shuleni na alijiunga na wanafunzi wenzake bila kulipa ada yoyote.

Karo ya shule ni Shilingi 35,000 kwa mwaka mzima.

"Kama shule, tumempatia sare na tunatamani kupata wahisani na viongozi ili kuhakikisha Odhiambo anasalia shule," alisema.