Mvulana aliyeketezwa na kaka zake aaga dunia

Muhtasari

- Mkurugenzi wa DCI George Kinoti alisema mvulana huyo alifariki mapema siku ya Jumatano kutokana na majeraha ya moto.

 

Pingu
Image: Radio Jambo

Mvulana mwenye umri wa miaka 14 ambaye alimwagiwa petroli na kuchomwa moto na kaka zake wakubwa amefariki.

Mkurugenzi wa DCI George Kinoti alisema mvulana huyo alifariki mapema siku ya Jumatano kutokana na majeraha ya moto alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kaunti ya Mandera.

“Alipigana kwa ujasiri kwa ajili ya maisha yake, lakini kuelekea saa 2 asubuhi ya leo, alikata tamaa na kwenda kuwa na Bwana. Baba yake Abdullah Hassan aliyefadhaika, ambaye hakukubali kufiwa na mwanawe mpendwa, alitokwa na machozi ya uchungu na huzuni aliporipoti kifo chake kwa maafisa wetu,” Kinoti alisema.

Mvulana huyo, mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi ya mtaani Mandera alichomwa moto na kaka zake wakubwa wakihofia kwamba anaweza kutoa ushahidi dhidi ya mmoja wao anayedaiwa kuiba simu ya rununu.

Mwanafunzi huyo wa darasa la saba katika Shule ya Msingi ya Kamor huko Mandera alishawishiwa hadi nyumbani kwao na kaka zake kabla ya kuviringishwa kwenye godoro lililomwagiwa petroli na kuchomwa moto.

Maafisa wa polisi walikuwa wamekimbilia nyumbani kwao huku moto ukiwaka siku iliyotangulia na kumuokoa mvulana huyo ambaye alikuwa ameungua vibaya sana.

Kinoti alisema wapelelezi wamewakamata ndugu hao - Ibrahim Ahmed Shaur, 20 na Yusuf Ahmed Shaur, 17 - ambao walikuwa wamejificha.

Kwa sasa wako katika kituo cha Polisi cha Mandera wakiendelea kushughulikiwa kwa kosa la mauaji kinyume na kifungu cha 203 kama kikisomwa na kifungu cha 204 cha kanuni ya adhabu.