Utapata Ulcers! Moses Kuria asihi rais Kenyatta akome kujihusisha na siasa za mpito

Kuria amemsihi rais awaruhusu wananchi wajiamulie wenyewe ambaye wangetaka awaongoze baada yake kustaafu

Muhtasari

•Kuria alimsihi rais Kenyatta kufuata nyayo za rais wa zamani Mwai Kibaki ambaye hakuwahi taja  yule ambaye angependelea aridhi kiti chake alipokuwa anastaafu takriban miaka nane iliyopita.

•Mwandani huyo wa naibu rais William Ruto alimshtumu rais  kwa kushurutisha wananchi wamchague Raila Odinga huku akidai kuwa kinara huyo wa ODM hana uwezo wa kunyakua kiti cha urais.

Mbunge wa Gatunndu Kusini, Moses Kuria
Moses Kuria Mbunge wa Gatunndu Kusini, Moses Kuria
Image: Courtesy

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria ameshauri rais Kenyatta kustaafu kwa amani na kuacha kujishughulisha na siasa za mpito za mwaka wa 2022.

Alipokuwa anazungumza akiwa katika kaunti ya Murang'a siku ya Jumamosi, Kuria alisihi rais kuachia viongozi wengine jukumu la kupanga nani atakayeridhi kiti cha urais mwaka ujao.

Kuria alimsihi rais Kenyatta kufuata nyayo za rais wa zamani Mwai Kibaki ambaye hakuwahi taja  yule ambaye angependelea aridhi kiti chake alipokuwa anastaafu takriban miaka nane iliyopita.

"Rais wetu lazima akuwe tayari kuturuhusu tujipange. Kujipanga pia ni haki yetu. Ugeni ni kama mto ambao unapoisha mtu hurudi nyumbani. Sasa yeye anaenda, ako na bahati tulimchagua mara tatu. Mimi natamani mngenichagua tu mara nusu. Tunachotaka ni aache kuingilia mambo ya siasa za mpito. Tafadhali achana nazo zitakuvunja moyo, hutawezana nazo, utapata vidonda vya tumbo, utapatwa na mchichimko na utavimbiwa kwa sababu ya mambo ambayo unaweza kuepuka. Kibaki hakujiingiza kwa maneno kama haya. Hakujalishwa na nani angekuja baada yake. Tunataka rais apumzike awe anakula vizuri kwa sababu amefanya kazi yake vizuri" Kuria alisema.

Kuria amemsihi rais asisumbuliwe tena na  suala la mridhi wa kiti chake huku akidai kwamba sio sharti kazi aliyokuwa amepanga kutekeleza ikamilike yote. Alieleza kuwa atakayeridhi kiti hicho ataendeleza kazi kutoka atakapokuwa ameachia.

Mwandani huyo wa naibu rais William Ruto alimshtumu rais  kwa kushurutisha wananchi wamchague Raila Odinga huku akidai kuwa kinara huyo wa ODM hana uwezo wa kunyakua kiti cha urais.

"Badala ya kupumzika na kustaafu vizuri unaanza kujiwekelea kazi ambayo itakupa msongo wa mawazo. Kazi nyingine ata haiwezekani, kama ya kujaribu kufanya Raila rais. Haiwezekani, heri uende ukachonge mawe kwa machimbo. Hiyo ni kazi ngumu sana" Kuria alisema.

Mbunge huyo amemsihi rais awaruhusu wananchi wajiamulie wenyewe ambaye wangetaka awaongoze baada yake kustaafu.