Oscar Sudi hakufanya mtihani wa KCSE mnamo mwaka wa 2006- Mahakama yaarifiwa

Muhtasari

•Shahidi aliambia hakimu Felix Kombo kuwa Sudi hakujiandikisha wala kukalia mtihani wa KCSE 2006 katika shule ya sekondari ya Highway iliyo jijini Nairobi.

•Kashu alisema kwamba baada ya uchunguzi walibaini kuwa nambari  401006 haikuwa ya shule ya sekondari ya Highway ila ilikuwa ya shule ya sekondari ya Parklands.

•Kashu alisema kuwa nambari 401006/081 ilikuwa ya Obaje Bob Onyango ambaye alikalia mtihani katika shule ya sekondari ya Parklands mwaka wa 2006.

Oscar Sudi
Oscar Sudi
Image: MAKTABA

Siku ya Jumanne mahakama ya kupambana na ufisadi iliambiwa kuwa mbunge wa Kapsaret Oscar Sudi hakufanya  mtihani wa KCSE mwaka wa 2006 kama ilivyodaiwa hapo awali.

Karani mkuu wa baraza la mitihani nchini (KNEC), Nabiki Kashu aliambia hakimu Felix Kombo kuwa Sudi hakujisajili kwa mtihani wa KCSE 2006 katika shule ya sekondari ya Highway iliyo jijini Nairobi.

Alikuwa anatoa ushahidi kwenye kesi ambapo Sudi anashtakiwa kwa kughushi cheti cha Diploma katika mafunzo ya usimamizi wa biashara ambacho alidai kupewa na taasisi ya usimamizi nchini (KIM).

Pia ameshtakiwa kwa kosa la kughushi cheti chake cha KCSE ambacho alidai kuwa cheti halisi cha KNEC.

Kashu ambaye ni shahidi wa nane alisema kwamba walipokea barua kutoka kwa EACC mnamo Septemba 15 wakiomba uthibitisho wa matokeo ya mtihani ya Sudi ya mwaka wa 2006.

"Kwenye barua hiyo tuliombwa kuthibitisha kama kwamba kuna mtahiniwa kama huyo aliyekalia mtihani wa KCSE katika shule ya sekondari ya Highway mnamo mwezi wa Novemba mwaka wa 2006 na kupokea cheti nambari 3381074, chini ya index 401006/081

Kashu alisema kwamba baada ya uchunguzi walibaini kuwa nambari  401006 haikuwa ya shule ya sekondari ya Highway ila ilikuwa ya shule ya sekondari ya Parklands. Kulingana na rekodi, nambari ya Highway ni 401005.

"Pia tuligundua kuwa hakuna rekodi ya mtahiniwa anayeitwa Sudi  aliyekaliwa mtihani katika shule ya sekondari ya Parklands ama ya Highway mnamo mwaka wa 2006" Shahidi alisema.

Mahakama iliarifiwa kuwa mnamo mwaka wa 2006 hakukuwa na shule ya upili iliyoitwa Highway kama ilivyokuwa imeandikwa kwa cheti cha Sudi.

Kashu alisema kuwa nambari 401006/081 ilikuwa ya Obaje Bob Onyango ambaye alikalia mtihani katika shule ya sekondari ya Parklands mwaka wa 2006.

"Hakuna uwezekano wa shule mbili kutumia nambari moja ya usajili kwa wakati mmoja wa mtihani. Pia hakuna uwezekano wa watahiniwa wawili kutumia nambari moja ya usajili" Kashu alisema.

Shahidi huyo alieleza mahakama kuwa vyeti ambavyo vilipelekwa kwa KNEC vilikuwa vimeghushiwa.

Kashu amekuwa akifanyia KNEC kazi kwa kipindi cha miaka 19. Majukumu yake ni pamoja na kuthibitisha matokeo ya mitihani, kubadilisha vyeti  na kusawazisha mitihani  ya kigeni.