Ndugu wawili ambao walichoma ndugu yao mdogo ambaye aliyeshuhudia mmoja wao akiiba simu wasakwa Mandera

Muhtasari

•Ibrahim Ahmed na Yusuf Ahmed walimshtumu ndugu yao mdogo kuwa shahidi katika kesi ambapo Ibrahim alikuwa anadaiwa kuiba simu

•Mwanafunzi huyo wa darasa la saba alidanganywa na ndugu zake wawili watundu aingie kwa nyumba yao ambapo walimfunga kwa gondoro kisha kuimwagilia mafuta na kuwasha moto.

crime scene 1
crime scene 1

Mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 14 alinusurika kifo baada ya polisi kumuokoa kutoka kwa moto uliokuwa umewashwa na ndugu zake wawili ambao walikusudia kumuua.

Inaripotiwa kwamba kijana huyo ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi ya Kamor, kaunti ya Mandera alidanganywa na ndugu zake wawili watundu aingie kwa nyumba yao ambapo walimfunga kwa gondoro kisha kuimwagilia mafuta na kuwasha moto.

Kulingana na DCI, Ibrahim Ahmed na Yusuf Ahmed walimshtumu ndugu yao mdogo kuwa shahidi katika kesi ambapo Ibrahim alikuwa anadaiwa kuiba simu.

Baada ya mpango wao wa kinyama kufanya kazi, wakorofi hao wawili walitoweka na kuenda mafichoni huku wakiacha ndugu yao mdogo achomeke hadi kifo.

Kwa bahati nzuri, polisi ambao walikuwa wameshika doria karibu na eneo la tukio waliona moto mkubwa ukitokea kwenye nyumba ile na wakakimbia pale kubaini kilichokuwa kinaendelea.

Polisi walipowasili kwenye eneo la tukio ndipo walipomuona kijana yule akichomeka na wakajitolea mhanga kumuokoa.

Baada ya mhasiriwa kuokolewa akiwa hali mahututi alikimbizwa katika hospitali ya rufaa ya kaunti ya Mandera ambako anaendelea kupokea matibabu.

Huku madaktari wakiendelea kumhudumia kijana yule, polisi kwa upande wao wanawasaka ndugu zake waliotekeleza kitendo hicho cha unyama.