Majonzi baada ya wanafunzi 4 wa chuo kikuu cha Tharaka waliokuwa wameenda kupiga picha mtoni kufa maji

Muhtasari

•Mashahidi walisimulia kwamba yote yalianza wakati mmoja wao alianza kuzama na wengine walipojaribu kumuoka wakazama pia na kufa maji.

•Msemaji wa polisi  Bruno Shioso alisema kundi la wanafunzi wa mwaka wa kwanza walikuwa wamekwenda mtoni kwa ajili ya kupiga picha ambapo baadhi yao waliamua kuogelea bila kujali hatari iliyowatazamia macho.

Image: FACEBOOK// THARAKA UNIVERSITY COLLEGE

Habari na Cyrus Ombati

Kipindi cha kupiga picha kiligeuka kuwa msiba baada ya wanafunzi wanne kutoka Chuo Kikuu cha Tharaka kufa maji walipokuwa wanaogelea katika mto Kathita alasiri ya Jumamosi.

Kufikia usiku wa Jumamosi, miili mitatu ilikuwa imetolewa majini tayari huku msako wa mwili wa nne ukiendelea.

Msemaji wa polisi Bruno Shioso alisema kuwa miili iliyopatikana ni ya wanaume wawili na  mwanamke mmoja huku akitaja tukio hilo kuwa msiba.

Alisema kuwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza walikuwa wanaogelea wakati wanne kati yao walikufa maji.

Mashahidi walisimulia kwamba yote yalianza wakati mmoja wao alianza kuzama na wengine walipojaribu kumuoka wakazama pia na kufa maji.

Wanafunzi wengine wawili waliweza kunusurika baada ya wakazi kuwaokoa na kuwakimbiza hospitalini.

Kwa bahati mbaya wenzao wanne waliwezwa na mikondo ya maji yenye nguvu na kupoteza maisha yao. Miili iliyopatikana ilipelekwa katika mochari ya Marimanti.

Shioso alisema kundi la wanafunzi wa mwaka wa kwanza walikuwa wamekwenda mtoni kwa ajili ya kupiga picha ambapo baadhi yao waliamua kuogelea bila kujali hatari iliyowatazamia macho.

Alisema kuwa wazazi wa wahasiriwa tayari walikuwa wamefahamishwa kuhusu tukio hilo la kuhofisha,