Polisi kutoa 50m kukamatwa kwa washukiwa 5 wa ugaidi

Muhtasari

• Idara ya DCI imetangaza kutoa jumla ya shilingi milioni 50 kwa mtu atakaetoa habari zitakazo pelekea kukamatwa kwa washukiwa watano wa ugaidi.

 

Elgiva Bwire Oliacha. Picha: MAKTABA
Elgiva Bwire Oliacha. Picha: MAKTABA

Idara ya DCI imetangaza kutoa jumla ya shilingi milioni 50 kwa mtu atakaetoa habari zitakazo pelekea kukamatwa kwa washukiwa watano wa ugaidi.

Katika taarifa yake DCI imesema watano hao ni watu hatari waliojihami na wanapanga kutekeleza mashambulizi nchini.

1. Salim Rashid Mohamed aka Chotara aka Turki

Salim alikuwa ameachiliwa kwa dhamana na anaaminika kujiunga na kundi la Daesh, kundi la kigaidi linaloendesha shughuli zake nchini Musumbiji.

Ni mzaliwa wa Mombasa na amehusishwa sana na visa kadhaa vya uhalifu. Kulingana na ripoti za kijasusi Salim anapanga kurejea nchini kutekeleza mashambulizi ya kigaidi.

2. Elgiva Bwire Oliacha aka Seif Deen Mohamed aka Japhar aka Japhel Okuku aka Abu Muadh

Aliachiliwa kutoka gereza la Kamiti tarehe 28/10/2021 baada ya kutumikia kifungo cha miaka 10 kwa kosa ka kushiriki shughuli za kigaidi.

Kulingana na taarifa ya DCI  Elgiva alikuwa ameahidi kutekeleza mashambulizi dhidi ya raia na maafisa wa usalama. Alienda mafichoni punde tu alipoachiliwa na inaaminika anapanga kutekeleza mashambulizi. Idara ya polisi inataka mtu yeyote aliye na ripoti kumhusu kujulisha polisi.

3. Birigi Abdikadir Haila

Kulingana na DCI Birigi amejiunga na kundi la Al Shabaab nchini Somalia hivi majuzi. Ni mzaliwa wa eneo la Manyatta, Moyale kaunti ya Mandera. Polisi wanasema amejihami kwa silaha na ni hatari na wananchi wametahadharishwa kumhusu.

4. Muhammad Abubakar alia Minshawary

Anashukiwa kujiunga na kundi la Al Shabaab nchini Somalia. Ni mzaliwa wa eneo la Kibokoni, Old town  kaunti ya Mombasa. Wananchi wametahadharishwa kumhusu.

5.Trevor Ndwiga aka idriss Jamal

Trevor ambaye alikuwa ameachiliwa kwa dhamana anaaminika kujiunga na kundi la Al Shabaab nchini Somalia.Anatoka eneo la Hamza, kaunti ndogo ya Makadara katika kaunti ya Nairobi.