Rais Kenyatta awasuta majaji wanaozuia wenzao kuchunguzwa

Muhtasari

•Alisema mahakama hazipaswi kutumia amri za mahakama kuepuka uwajibikaji akisema hiyo si demokrasia bali ni ubabe wa mahakama.

•Aidha rais alisema imebainika kuwa huenda maafisa wa mahakama wanahubiri maji lakini wanakunywa mvinyo wakidai kutoka kwa wengine kile ambacho hawako tayari kujifanyia.

•Alisema Wakenya wanatarajia mahakama mahiri na huru ambayo itazungumza ukweli  kwa njia ya haki, thabiti na inayowajibika

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amewasuta majaji ambao hutoa maagizo ya kuwakinga wenzao dhidi ya kufanyiwa uchunguzi.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na AG Kihara Kariuki wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Hali ya Mahakama na Utawala wa Haki (SOJAR) 2020/2021, rais amesema maafisa wa mahakama wanatumia afisi zao kuzuia serikali kuwachunguza.

Rais alisema majaji hutumia afisi zao kuzima uchunguzi wowote kuhusu mienendo yao "Bi hakimu mkuu, Wakenya hawakutarajia haya wakati walipigia katiba mpya kura kwa mamilioni,"

Alisema mahakama hazipaswi kutumia amri za mahakama kuepuka uwajibikaji akisema hiyo si demokrasia bali ni ubabe wa mahakama.

"Katika siku za hivi majuzi, mazungumzo ya hadhara ya bi hakimu mkuu yamekumbwa na madai ya kuegemea upande wa maamuzi ya maafisa wa mahakama ambayo hayazingatii matarajio ya agano letu takatifu," Kenyatta alisema.

Aidha rais alisema imebainika kuwa huenda maafisa wa mahakama wanahubiri maji lakini wanakunywa mvinyo wakidai kutoka kwa wengine kile ambacho hawako tayari kujifanyia.

"Haijapotea kwa Wakenya kwamba hali ya maamuzi ya hivi majuzi ya mahakama imekuwa na athari ya kusema maafisa wa mahakama hawawezi kuwajibika au kuwa chini ya sheria sawa na ambazo maafisa wengine wa umma wanashikiliwa," alisema.

Rais aliendelea kusema kama nchi hatuwezi tena kuwa na mahakama inayosema "tufanye tunavyosema si kama tufanyavyo au ambayo inazungumza kwa ujasiri kuhusu matawi mengine ya serikali lakini haitaruhusu kukabiliana na hata hatua za msingi za uwajibikaji,"

"Ni vipi mahakama inaweza kuwa na sauti ya kuaminika na zaidi ya kusimamia kesi za ufisadi wakati inazuia watu wake kutoka kwa viwango vya uwajibikaji vilivyotumika kwa wengine?" alisema.

Rais alihoji ni kwa namna gani nchi itapambana na ufisadi ikiwa theluthi kamili ya serikali haiko tayari kukabiliana na uozo ndani ya safu yake.

Huku akimpongeza Martha Koome kwa kuwa hakimu mkuu wa kwanza mwanamke, Kenyatta alisema ni lazima ripoti ya SOJAR iwe ukumbusho wa mara kwa mara kwamba mamlaka ya mahakama haitumiki kwa kiholela.

"Lazima mahakama iheshimu matakwa ya watu kushikilia urithi na mila zetu pamoja na kujifunga kikamilifu kwa upeo na mipaka ya majukumu iliyokabidhiwa kwake na watu wa Kenya," alisema.

Alisema Wakenya wanatarajia mahakama mahiri na huru ambayo itazungumza ukweli  kwa njia ya haki, thabiti na inayowajibika.

"Kama vyombo na mashirika mengine, mahakama lazima itarajie na kukaribisha maoni ya Wakenya kuhusu hatua na maamuzi yake hakuna kitengo cha serikali ambacho hakifai kukosolewa” Rais alisema