Mzozo wa ardhi: Jamaa amuua kakake Siaya

Muhtasari

• Kulingana na naibu chifu Ezekiel Ochieng Owino, mwili wa marehemu ulipatikana mbele ya nyumba ya marehemu mamake.    

• Mtoto wa marehemu alisema Alila alipigiwa simu kutoka nyumbani na kakake mwendo wa saa nne usiku wakati familia ilikuwa ikijiandaa kulala.  

Pingu
Image: Radio Jambo

 Uhasama baina ya kaka wawili kuhusu ardhi uliishia kwa mauti baada ya mmoja wa kaka hao kuawa katika kijiji cha Achiewo katika lokesheni ndogo ya Nyang’oma Kogelo kaunti ya Siaya.

             Joseph Alila Hamisi, mwenye umri wa miaka 48, alipatikana siku ya Alhamisi akiwa amelala kwenye kidimbwi cha damu muda mfupi baada ya majibizano na kaka yake aliyedaiwa kumwita kutoka nyumbani kwake.              

Kulingana na naibu chifu wa eneo la Nyang’oma Kogelo, Ezekiel Ochieng Owino, mwili wa marehemu ulipatikana mbele ya nyumba ya marehemu mamake.             

Owino alisema kuwa mtoto wa marehemu alisema Alila alipigiwa simu kutoka nyumbani na kakake mwendo wa saa nne usiku wakati familia ilikuwa ikijiandaa kulala.             

"Mtoto huyo anasema baba yake alipotoka, kaka yake alimpiga kwa rungu," alisimulia naibu wa chifu na kuongeza kuwa watoto hao walisema walisikia zogo lakini waliamua kujifungia ndani kwa hofu.             

Chifu huyo msaidizi alisema wanashuku kuwa mzozo wa ardhi uliodumu kati ya wawili hao ulikuwa chanzo cha mauaji hayo.             

Owino alisema marehemu alikuwa akikaa peke yake na watoto baada ya mkewe kutoroka.              Alisema kuwa mwili wa marehemu ulichukuliwa na polisi na unatarajiwa kufanyiwa upasuaji.  Majirani walikuwa na wasiwasi kuhusu maslahi ya watoto wa marehemu ambao sasa walikuwa wamesalia bila mzazi yeyote.                

Msako wa kumtafuta mshukiwa wa mauaji, ambaye alikwenda mafichoni unaendelea.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO