"Alikuwa rafiki na mshauri" DP William Ruto amuomboleza askofu maarufu Godfrey Migwi

Aliangamia kutokana na shinikizo la damu.

Muhtasari

• Ruto  amemtaja marehemu kama kiongozi wa dini jasiri, aliyekuwa na uwezo mkubwa na mcheshi.

•Mtumishi huyo wa Mungu alikuwa ametangaza azma ya kuwania kiti cha ubunge cha Mathioya, kaunti ya Muranga.

Marehemu Godfrey Migwi
Marehemu Godfrey Migwi
Image: FACEBOOK

Asubuhi ya Alhamisi Wakenya wameamkia habari za kusikitisha kuhusu kifo cha askofu maarufu Godfrey Migwi wa kanisa la House of Hope.

Askofu Migwi ambaye alijihusisha sana na siasa alifariki siku ya Jumatano. Inaripotiwa mtumishi huyo wa Mungu aliangamia kutokana na shinikizo la damu.

Wakenya wamefurika mitandaoni kumuomboleza Migwi huku wakifariji familia, waumini na marafiki wa marehemu.

Naibu rais William Ruto  amemtaja marehemu kama kiongozi wa dini jasiri, aliyekuwa na uwezo mkubwa na mcheshi.

Ruto amesema  marehemu alikuwa rafiki mkubwa na mshauri wake huku akidai watu watapeza sanan mahubiri yake.

"Bishop Migwi alikuwa jasiri, mwenye sauti na kiongozi wa dini mwenye nguvu na mcheshi.

 Alikuwa mshauri na rafiki aliyekuwa na imani ya uchungaji ambao alitia kwa wengi wetu. Tutapeza mahubiri yake yenye manufaa" Ruto alisema.

Amefariji familia, wapendwa na waumini wa kanisa la House of Hope huku akitakia marehemu mapumziko ya amani.

Mtumishi huyo wa Mungu alikuwa ametangaza azma ya kuwania kiti cha ubunge cha Mathioya, kaunti ya Muranga.