Polisi wanasa bangi yenye thamani ya shilingi milioni 6 Nyandarua

Muhtasari

•Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Nyandarua Dahir Mohamed , mihadarati hiyo ilikuwa ikisafirishwa kutoka Nakuru kuelekea Mombasa.

Bangi
Bangi
Image: MAKTABA

Siku ya Jumamosi polisi katika Kaunti ya Nyandarua walinasa bangi yenye thamani ya mtaani inayokadiriwa kufikia Sh6 milioni, katika nyumba ya kibinafsi huko Ol Kalou.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Nyandarua Dahir Mohamed , mihadarati hiyo ilikuwa ikisafirishwa kutoka Nakuru kuelekea Mombasa.

Bosi huyo wa polisi alisema polisi waliwasimamisha washukiwa waliokuwa wakisafirisha bangi katika barabara ya Ol Kalou - Njabini lakini wakaendelea na safari yao kwa kasi.

Baadaye walitelekeza gari hilo katika makao ya kibinafsi mjini Ol Kalou kabla ya polisi kufahamishwa na mwananchi.

Bw Dahir alisema kuwa bangi ilikuwa ikisafirishwa kwa Toyota Wish na ilikuwa imerundikwa kwenye magunia.

Alisema mshukiwa mmoja alikamatwa baadaye akijaribu kutoroka kwa miguu. Mshukiwa ataendelea kuzuiliwa na polisi na watafikishwa mahakamani Jumatatu.

Alisema bangi hiyo itakabidhiwa kwa timu ya kupambana na dawa za kulevya kwa tathmini zaidi.

Barabara hiyo hutumiwa sana na walanguzi wa dawa za kulevya kwani ni rahisi kuingia katika kaunti zingine jirani.

(Utafsiri: Samuel Maina)