Taifa gizani - Waziri asisitiza mageuzi katika Kenya Power

Muhtasari

• Waziri wa Kawi Monica Juma ameelezea haja ya kufanyika kwa mageuzi katika kampuni ya kusambaza umeme nchini Kenya Power. 

Minara iliyosababisha hitilafu katika nyaya za umeme
Minara iliyosababisha hitilafu katika nyaya za umeme
Image: HISANI

Waziri wa Kawi Monica Juma ameelezea haja ya kufanyika kwa mageuzi katika kampuni ya kusambaza umeme nchini Kenya Power. 

Alikuwa akijibu maswali kuhusu kukosekana kwa nguvu za umeme kwa siku mbili kutokana na hitilafu katika nyaya za umeme. 

Katika msururu wa jumbe za twitter siku ya Alhamisi, Juma alisema kukatika kwa umeme kunasisitiza 'lazima na uharaka' unaohitajika kwa mageuzi hayo. 

"Hii itahakikisha upatikanaji wa umeme thabiti na wa kutegemewa," alisema. 

"Wizara ya kawi iki mbioni kuhakikisha kwamba masaibu ya siku mbili zilizopita hayarudiwi." 

Juma aliipongeza KPLC na Kampuni ya Kusambaza Umeme ya Kenya (KETRACO) ambao walifanya kazi usiku kucha kurekebisha hitilafu na kurejesha umeme kote nchini. "Ninatoa wito kwa Wakenya wote, taasisi, wafanyikazi katika sekta ya nishati na washirika wetu kuunga mkono mageuzi haya," alisema. 

Kampuni ya Kenya Power ilisema hitilafu kwenye gridi yake ya taifa ilitokea baada ya minara inayotumia njia ya umeme yenye nguvu ya juu inayounganisha Nairobi na bwawa la Kiambere kuporomoka. 

Mwaka 2021, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i alisema Serikali itatekeleza mageuzi yaliyopendekezwa na jopo kazi lililoteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi mwaka huu kwenye KPLC. 

Jopokazi la KPLC lililaumu gharama ya juu ya umeme nchini kutokana na kandarasi ambazo zilifaidi sana wazalishaji huru wa umeme kwa gharama ya KPLC na watumiaji na kupendekeza kukaguliwa upya kwa kandarasi zote hizo ndani ya miezi minne.