Mshukiwa wa 'Wash Wash' akamatwa baada ya kulaghai mwekezaji Sh800,000

Washukiwa walipatikana na sanduku zito, jeusi, la chuma.

Muhtasari

•Uchunguzi wa awali  umebaini kuwa kwa kawaida Babila  huwashawishi wateja wake kwa kuwadanganya kwamba watapata pesa za haraka kwa kusafisha dola zao bandia na kuzifanya  kuwa pesa halisi.

•Mwekezaji kutoka Australia anayefanya biashara nchini Kenya na Dubai alianguka kwenye mtego na kuwapatia matapeli hao Ksh800,000 kabla ya kugundua baadae kwamba amechezwa.

Image: TWITTER/// DCI

Polisi jijini wanamzuilia jamaa mmoja kufuatia madai kwamba alijipatia pesa kwa njia laghai  kutoka kwa mwekezaji mmoja kutoka Australia anayeishi hapa nchini.

Timson Tiekam Babila ambaye ni mzaliwa wa Cameroon alikamatwa na maafisa wa kitengo cha Upelelezi Wa Jinai (DCI)  katika hoteli moja iliyo eneo la Kilimani mnamo Alhamisi baada yao kudokezewa na mlalamishi.

DCI wameripoti kwamba Babila alikamatwa pamoja na wenzake wawili, Ernest Abeng Ahuo na Ayong Ronald Aku ambao wote ni raia wa Cameroon wanaoaminika kuendeleza biashara laghai ya 'wash wash'.

Uchunguzi wa awali  umebaini kuwa kwa kawaida Babila  huwashawishi wateja wake kwa kuwadanganya kwamba watapata pesa za haraka kwa kusafisha dola zao bandia na kuzifanya  kuwa pesa halisi.

Ili kufanikisha hili, mshukiwa kwanza huwaomba wahasiriwa wake fedha halisi kwa ajili ya ununuzi wa kemikali na vifaa vingine vinavyotumika kusafisha noti hizo bandia. Kwa kawaida huwa ni masanduku ya chuma yaliyofungwa.

Mwekezaji kutoka Australia anayefanya biashara nchini Kenya na Dubai alianguka kwenye mtego na kuwapatia matapeli hao Ksh800,000 kabla ya kugundua baadae kwamba amechezwa.

Kufuatia hayo, mwekezaji huyo alipiga ripoti katika ofisi za maafisa wa ECCU jijini Nairobi akitumai kurejeshewa pesa zake.

Wapelelezi walimwekea mshukiwa mtego katika hoteli moja na wakaweza kuwatia mbaroni walipokuwa wanaingia mle ndani.

Washukiwa walipatikana na sanduku zito, jeusi, la chuma.

Mshukiwa huyo na washirika wake wanaishi katika mtaa wa  Ruaka, kaunti ya Kiambu, eneo ambalo limekuwa na washukiwa wengi wa  ‘Wash Wash’, ambao wanaishi maisha ghushi baada ya kuiba kutoka kwa wafanyabiashara wenye bidii.

Kwa sasa watatu hao wanaendelea kuzuiliwa huku wakisubiri kukamilika kwa hatua za kisheria.