Uhuru aambia mahakama kuwa hawezi kushtakiwa akiwa rais

Muhtasari

• Rais Kenyatta, kupitia Wakili Waweru Gatonye, ​​anasema mahakama za chini zilikosea kisheria kwa kupata kwamba anaweza kushtakiwa.

• Gatonye alidai kuwa kumshtaki Rais ni njia ya kumuondoa katika kutekeleza majukumu yake.

• Alisema ikiwa dhana hii itachukuliwa vile ilivyo huenda ikafika wakati mahakama ikamtaka Rais kufika mahakamani na kujibu mashtaka dhidi yake.

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amesema ana kinga kamilifu na hawezi kushtakiwa kwa kutekeleza majukumu ya urais.

Katika siku ya pili ya kusikilizwa kwa kesi ya BBI iliyoanza Jumanne, Rais Kenyatta, kupitia Wakili Waweru Gatonye, ​​anasema mahakama za chini zilikosea kisheria kwa kupata kwamba anaweza kushtakiwa.

Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu iliamua kwamba Rais anaweza kushtakiwa kwa nafasi yake binafsi katika kipindi chake cha uongozi kwa jambo lolote alilofanya au kutofanya.

Gatonye aliambia mahakama kwamba mahakama ya rufaa ilifikia uamuzi huo ingawa Rais alikuwa ameshtakiwa si kuhusiana na suala la kibinafsi bali kwa kile alichofanya akiwa kiongozi wa nchi.

Gatonye aliendelea kusema kwamba kulingana na sheria rais Rais au mtu anayetekeleza majukumu ya ofisi hiyo katika kipindi cha uongozi wake hawezi kamwe kushtakiwa kwa jambo lolote lililofanywa au kutofanywa katika utekelezaji wa mamlaka yake.

Alidai kuwa kumshtaki Rais ni njia ya kumuondoa katika kutekeleza majukumu yake.

"Iwapo ingeruhusiwa kwa kila mtu kuwasilisha kesi dhidi ya Rais, ingemsumbua katika kutekeleza majukumu muhimu zaidi ya kuendesha serikali," Gatonye alisema.

Alisema moja ya sababu za kinga ya Rais ni kulinda usalama wa taifa, na ipo haja ya kulinda heshima ya Ofisi ya Rais.

"Haiwezi kutiliwa shaka, lakini kuna vyombo vikuu vitatu vya serikali na muundo wetu wa kikatiba, na taasisi hizo zinahitaji kufanya kazi kwa heshima ili umma uweze kuwa na imani nao," alisema.

Alisema ikiwa dhana hii itachukuliwa vile ilivyo huenda ikafika wakati mahakama ikamtaka Rais kufika mahakamani na kujibu mashtaka dhidi yake.

Kuhusu suala la iwapo Rais anaweza kuanzisha mchakato wa kubadilisha katiba, Wakili Kiragu Kimani alisema mahakama ilikosea kuona kuwa Rais hawezi kuanzisha mchakato huo.