Uhaba mkubwa wa kondomu washuhudiwa Kenya

Muhtasari

•Hali hii imeweka wananchi katika hatari kubwa ya mimba zisizotarajiwa pamoja na kuambukizwa virusi vya ukimwi na maradhi mengine ya zinaa.

•Uhaba huu umelazimu NACC kuangazia zaidi watu ambao wanahitaji mipira hiyo ambayo kwa miaka serikali imekuwa ikiisambaza bure.

Kenya yakabiliwa na uhaba wa kondomu
Kenya yakabiliwa na uhaba wa kondomu
Image: BBC

Nchi ya Kenya imekabiliwa na uhaba mkubwa wa mipira ya kondomu  katika siku za hivi karibuni, Baraza  la Kudhibiti Ukimwi nchini (NACC) limesema.

Hali hii imeweka wananchi katika hatari kubwa ya mimba zisizotarajiwa pamoja na kuambukizwa virusi vya ukimwi na maradhi mengine ya zinaa.

NACC imesema akiba ya taifa imesalia na kondomu milioni 79 pekee ilhali mahitaji ya kondomu nchini yanafikia milioni 480 kila mwaka.

Alipokuwa anazungumza katika hafla ya kuadhimisha siku ya Kondomu Duniani iliyoandaliwa katika chuo cha Kenya Coast Polytechnic siku ya Jumapili, mkuu wa baraza la NACC katika eneo la Pwani Omar Mwanjama alisema uhaba wa kondomu katika akiba ya taifa umeathiri ugavi wa bure wa mipira hiyo. 

Mwanjama alisema kwamba serikali inajikakamua kuhakikisha kwamba mipira hiyo muhimu imepatikana hivi karibuni.

"Uhaba wa kondomu ni wa kweli na unahitaji kushughulikiwa kwani unaweza kupunguza kasi ya vita  dhidi ya ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa,”  Mwanjama alisema.

Hali hii imelazimu NACC kuangazia zaidi watu ambao wanahitaji mipira hiyo ambayo kwa miaka serikali imekuwa ikiisambaza bure.

Siku chache zilizopita NACC ilitangaza kwamba mamilioni ya mipira ya kondomu inatarajiwa kuwasili nchini mwezi ujao.