Ruto aendelea kuongoza, Raila aongeza umaarufu- TIFA

Muhtasari

•Matokeo ya utafiti huo ambayo yaliachiliwa asubuhi ya Alhamisi yameashiria kwamba Ruto anaongoza na 38.7% ilhali kinara wa ODM anafuata na 27%.

Kiongozi wa Azimio la Umoja Movement Raila Odinga na Naibu Rais na kiongozi wa chama cha UDA William Ruto.
Kiongozi wa Azimio la Umoja Movement Raila Odinga na Naibu Rais na kiongozi wa chama cha UDA William Ruto.
Image: THE STAR

Utafiti wa TIFA wa hivi majuzi umebaini kuwa naibu rais William Ruto ndiye anayependelewa zaidi kuwa rais katika kinyang'anyiro cha mwezi Agosti.

Matokeo ya utafiti huo ambayo yaliachiliwa asubuhi ya Alhamisi yameashiria kwamba Ruto anaongoza na 38.7% ilhali kinara wa ODM anafuata na 27%.

Utafiti huo umeashiria kwamba umaarufu wa naibu rais umesalia sawa  tangu mwezi Novemba ilhali Raila ameongeza umaarufu kwa asilimia 4.

Asilimia 20 bado hawajafanya maamuzi yao ilhali 10% ya waliohojiwa walikosa kutoa majibu.

Umaarufu wa Ruto katika eneo la Mlima Kenya kwa sasa unasimamia katika asilimia 49 ilhali Raila anashabikiwa na asilimia 20.

Asilimia 16 katika eneo hilo bado hawajafanya maamuzi.

Utafiti huo unaashiria kuwa Ruto amepoteza pointi nne katika eneo la kati ilhali Raila ameongeza katika eneo hilo. 

Utafiti huo ulifanyika baada ya matukio  mawili makubwa ya kisiasa kufanyika katika kipindi cha miezi mitatu ambacho kimepita.

Raila alitangaza kuwa atawania kiti cha urais mwezi Agosti. Musalia Mudavadi na Moses Wetangula walijiunga na kambi ya Ruto.

"Haya ni matukio mawili ambayo yameathiri matokeo yetu" Ilisemwa.

Licha ya Mudavadi na Wetangula kujiunga na Ruto, Raila aliongeza umaarufu katika eneo la Magharibi kwa pointi 10 ilhali Ruto aliongeza kwa pointi 2.

Chama cha Ruto, UDA ndicho maarufu zaidi kikiwa na asilimia 35 kikifuatwa nyuma na ODM ambacho kina asilimia 24.

Umaarufu wa ODM umeongezeka mara dufu kutoka asilimia 12 iliyotangazwa mnamo Juni 2020.

Chama cha Wiper kina asilimia 2 huku ANC na Ford Kenya zikiwa na asilimia 1 kila mmoja.