Raila Odinga 'government project!' Uhuru asitisha kimya chake

Muhtasari

• Rais Uhuru Kenyatta amesema hana mtu yeyote ambaye atamzindua kama mradi wa serikali kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na baadhi ya viongozi katika kampeni mbali mbali kote nchini.

Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta amesema kwamba yeye ni mkenya kama wengine na ana haki ya kufanya maamuzi yake kuhusu muelekeo wa siasa za taifa.

Akizungumza siku ya Jumatatu katika kaunti ya Mombasa, rais Kenyatta alisema kwamba kuna wale ambao wamekuwa wakidai kuwepo kwa mradi wa serikali  katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu ujao huku akidai kwamba hakuna tatizo lolote iwapo jambo hilo lingetokea.

"Ubaya wa mradi wa serikali ni upi?"Kenyatta aliuliza.

Uhuru alisema kwa sasa anafanyia wakenya kazi  na wakati utafika ambapo yeye kama mkenya pia atatoa  mwelekeo kuhusu mustakabali wa siasa za taifa hili.

Alipuuzilia mbali wale ambao wamekuwa wakidai kuwa chama cha Jubilee kimekufa akisema kwamba serikali iliyoko ni ya Jubilee na wakati utafika wataungana na wengine kuendeleza gurudumu la taifa. 

“Mimi nina kura moja tu kama mkenya mwingine, wakati utafika ambapo mimi na wachache watakaokubaliana na mimi pia tutatoa mwelekeo”, Uhuru alisema.

Naibu rais William Ruto na wafuasi wake wamekuwa wakidai kuwa kinara wa ODM ni mradi wa serikali ambao unashinikizwa na rais Kenyatta na mabwenyenye nchini kwa lengo la kulinda mali zao.

Rais Kenyatta alisema kwa sasa hana muda wa kuwajibu wanaomtusi kwa sababu anawatumikia wananchi.

Kulingana na rais kazi hufanyika kwa ofisi sio kwa mikutano ya kisiasa.

Huku akionekana kumzungumzia naibu rais William Ruto Uhuru alisema kwamba kuna viongozi walichaguliwa kuhudumia wakenya ila wamezama katika siasa zisizo za maendeleo.

Akizungumza katika uzinduzi wa mpango wa afya kwa wote, Kenyatta alisema hata yeye ni Mkenya  na kura yake ni moja tu na atampigia mwaniaji wa urais atakayempendelea kama ilivyo haki ya kila mkenya.

Kenyatta amesema kwamba wale wanaomshambulia pamoja na kueneza uvumi kwamba chama tawala cha Jubilee kimefifia na kupoteza umaarufu wake ni wanafiki tu ambao wanaendeleza porojo na propaganda kwenye mikutano ya kisiasa badala ya kufanya kazi ambazo walichaguliwa kutimiza, akionekana kuwashambulia wanasiasa wa mrengo wa Kenya Kwanza ambao wamekuwa wakimshambulia kwamba anatumia kinara wa ODM Raila Odinga kama mradi wa serikali.