Serikali kuharamisha kundi la wapiganaji Pokot magharibi

Muhtasari

• Serikali kuu sasa inatarajiwa kukitangaza kikundi cha wapiganaji wa kaunti ya Pokot magharibi kuwa haramu.

• Matiang’i alisema kwamba tayari kuna mikakati iliyowekwa na polisi ili kuleta usalama eneo hilo ila kundi hilo linazidi kutifua mipango hiyo kila mara

Waziri Fred Matiang'i
Waziri Fred Matiang'i
Image: Ezekiel Aming'a

Serikali kuu sasa inatarajiwa kukitangaza kikundi cha wapiganaji wa kaunti ya Pokot magharibi kuwa haramu.

Kundi hilo loimelaumiwa kwa mashambulizi kadhaa katika eneo la kaskazini mwa bonde la ufa ambayo yamelekea vifo vya watu kadhaa, wengine kujeruhiwa na kufurushwa makwao.

Waziri wa usalama wa kitaifa, Fred Matiang;i alisema kwamba kuanzia wiki ijayo atatoa pendekezo kwa baraza la usalama wa taifa kwamba wapiganaji hao wa kaunti ya Pokot magharibi watangazwe kuwa kundi haramu.

“Kutangazwa kwao kuwa kundi haramu kutasaidia serikali kutumia nguvu zaidi kufanya upelelezi wa kina kuhusu wapigananji hao,” Matiang;’i alisema.

Matiang’i alisema kwamba tayari kuna mikakati iliyowekwa na polisi ili kuleta usalama eneo hilo ila kundi hilo linazidi kutifua mipango hiyo kila mara.

Vilvile huenda amri ya kutokuwa nje ikadumishwa katikaeneo hilo ili kuleta hali ya utulivu.

Kundi hilo limekuwa likifanikisha mashambulizi ya mara kwa mara na baadaye kuwapora mifugo wa wakazi katika eneo hilo.

Matiang’i alizungumza haya katika eneo la Kabete ambapo pamoja na waziri wa elimu Geroge Magoha walikuwa wakiwakabidhi wakurugenzi wa mitihani funguo na kufuli za makonteina ya kuhifadhi karatasi za mitihani ya kitaifa.

Aidha waziri huyo amewaonya wakuu wote wa shule dhidi ya kuruhusu mabasi ya shule kufanya safari baada ya 6:30 jioni akisema kwamba watachukuliwa hatua kali za kisheria.