Sitamuunga Ruto mkono, lazima abadili mienendo - Uhuru

Muhtasari

• Rais Uhuru Kenyatta kwa mara ya kwanza amesema wazi kwamba hatamuunga mkono naibu rais William Ruto kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

• Rais ametangaza kwamba atakuwa anampigia debe kinara wa upinzani ambaye pia ni kiongozi wa mrengo wa Azimio, Raila Odinga katika uchaguzi mkuu ujao.

 

Andrew Kasuku
Andrew Kasuku
Image: KWA HISANI

Rais Uhuru Kenyatta kwa mara ya kwanza amesema wazi kwamba hatamuunga mkono naibu rais William Ruto kwa uchaguzi mkuu wa 2022.

Akizungumza na wajumbe wa Jubilee siku ya Jumatano  katika eneo la Sagana, rais hata hivyo alisema kwamba huenda akamuunga Ruto mkono katika chaguzi zijazo ikiwa atabadili mienendo yake.

Rais alisema kwamba vijana wamekuwa wakipotoshwa na kuambiwa mambo ya uongo  kwa kutumia pesa ambazo zimepatikana kwa njia za  ufisadi , “…pesa za Arror na Kimwarer.”

Rais ametangaza kwamba atakuwa anampigia debe kinara wa upinzani ambaye pia ni kiongozi wa mrengo wa Azimio, Raila Odinga katika uchaguzi mkuu ujao.

Uhuru aliiomba jamii yake ya mlima Kenya kuunga mkono azma ya Raila Odinga akisema kwamba ana mipango bora ya kuimarisha maisha ya  wananchi.

Aidha akimrejelea naibu wake William Ruto, rais alisema kwamba hana shida kumuunga mkono katika siku zijazo ikiwa atabadilika.

“Ninawaomba muunge mkono Raila Odinga kwani ana maono mazuri kwa taifa. Kijana wangu atakapobadilika, tutafikiria mambo yake," Uhuru alisema.