Rais Kenyatta afunguka kuhusu sababu kuu za kufanya kazi na Raila

Muhtasari
  • Kenyatta alisema sababu yake kuu kumwalika kinara huyo wa ODM serikali ni kwa minajili ya amani
  • Alisema alimuomba Raila washirikiane pamoja ili kutafuta amani ila akamfahamisha kuhusu makubaliano yaliyokuwepo tayari kati yake na naibu wake William Ruto
Rais Uhuru Kenyatta
Image: Andrew Kasuku

Rais Uhuru Kenyatta amefunguka kuhusu sababu zake za kupungiana mkono na Raila na kukubali kufanya naye kazi.

Akizungumza katika kongamano la viongozi wa Mt Kenya ambalo liliandaliwa Sagana siku ya Jumatano, Kenyatta alisema sababu yake kuu kumwalika kinara huyo wa ODM serikali ni kwa minajili ya amani.

Rais alipuuzilia mbali madai kuwa alimtafuta Raila ili aweze kurithi kiti chake. Alisema kwamba haja yake kuu ni  kuacha nchi kwenye mikono salama.

"Sikufanya handshake kwa sababu nataka awe rais, nilitaka amani. Matamanio yangu ni jinsi nchi itakuwa baada ya kuondoka" Rais alisema.

Rais Kenyatta alifichua kuwa aliamua kumtafuta kinara huyo wa ODM kwa majadiliano kufuatia mtafaruko uliotokea nchini baada ya uchaguzi wa 2017.

Alisema alimuomba Raila washirikiane pamoja ili kutafuta amani ila akamfahamisha kuhusu makubaliano yaliyokuwepo tayari kati yake na naibu wake William Ruto.

"Nilikuwa namtukana nikimuita 'Kimundu' (Kimtu). Wazazi wangu walinifunza kutodanganya. Niliamua kumtafuta, mlinichagua ili niwalinde.. Nilimwambia kuwa tayari tuko na makubaliano na wengine" Uhuru alisema.

Rais alikosoa naibu rais na wandani wake kwa kukosoa hatua yake ya kufanya kazi na Raila huku akisema uamuzi  huo ulikuwa kwa manufaa ya nchi yote.