Gavana Ann Kananu akanusha madai ya kuwa mlevi

Muhtasari

Gavana wa Nairobi Ann Kananu amewakosoa baadhi ya wakilishi wadi wa City Hall ambao walimkashifu kwa kuwa mlevi.

Kananu alijitetea akisema kuwa mbali na kuwa Gavana pia yeye ni mfanyabiashara na amewekeza kwenye vilabu kadhaa vya usiku.

Alipuuza matamshi ya wenzake, akisema majukumu ya MCAs hayajumuishi kuangalia jinsi gani, lini na wapi maafisa wa wakuu wa kaunti wanajivinjari. 

Gavana wa Nairobi Ann Kananu amewakosoa baadhi ya wakilishi wadi wa City Hall ambao walimkashifu kwa kuwa mlevi.

Alisema wakilishi wadi hao walikuwa wakitumia jina lake kwa nia mbaya kusalia kuwa muhimu wakati wa msimu wa kampeni.

Wiki jana, wajumbe wawili wa bunge la kaunti walimkashifu Gavana wa Nairobi kwa kutojali wakazi wa Nairobi na uzembe.

MCA wa Waithaka Anthony Kiragu na mwenzake kutoka Utalii walidai kuwa Kananu alikuwa akionekana kila mara kwenye baa na vilabu vya usiku lakini si afisini kusaidia wakazi wa Nairobi.

“Yeye ni gavana ambaye hayupo. Kananu hayuko ofisini kamwe. Anadaiwa kuwa mlevi na kwamba kila mara anakunywa pombe kwenye vilabu vya usiku,” Kiragu alisema.

Akiongea na Star, Kananu alijitetea akisema kuwa mbali na kuwa Gavana pia yeye ni mfanyabiashara na amewekeza kwenye vilabu kadhaa vya usiku.

“Ninamiliki biashara kadhaa, zikiwemo vilabu vya usiku jijini Nairobi na kaunti zingine. Na kama mkurugenzi wa vilabu mbalimbali vya usiku, nina haki ya kutembelea eneo la biashara yangu na kujua jinsi zinavyosimamiwa. Je, hilo linanifanya kuwa mlevi?” aliuliza.

Gavana huyo alieleza zaidi kwamba amekuwa akimiliki vilabu hivyo vya usiku kwa miaka minne sasa na haijawahi kumuingilia katika kazi yake ya City Hall.

Kananu aliongeza kuwa anadhibiti na amejitolea kikamilifu kuwahudumia wakazi wa Nairobi katika ngazi ya kaunti.

“Kama Gavana, unafanya kazi zaidi ya muda unaotakiwa na baadhi ya mikutano yangu naifanya katika maeneo yangu ya biashara. Hii haimaanishi kuwa mimi ni mlevi… naongoza mikutano yangu ya kila wiki ya baraza la mawaziri na kuhudhuria hafla na mikutano ninapohitajika.” 

Gavana alitoa wito kwa MCAs kuzingatia utoaji wa huduma na kuachana na propaganda. 

"Tunafanya kazi hadi saa kumi na moja jioni katika Jumba la Jiji. Hebu tuangazie wakazi wa Nairobi," Kananu aliongeza. 

Baadhi ya MCAs wa Nairobi pia walijitokeza kumtetea gavana huyo kuhusu madai yaliyotolewa na wenzao. Wakiongozwa na MCA wa Imara Daima Kennedy Obuya, MCAs kutoka vyama vyote viwili vya Jubilee na ODM walikashifu mashambulizi dhidi ya Kananu, wakisema kwamba Gavana hapaswi kuhadaiwa na kuharibiwa jina kwa sababu za kibinafsi. 

Alipuuza matamshi ya wenzake, akisema majukumu ya MCAs hayajumuishi kuangalia jinsi gani, lini na wapi maafisa wa wakuu wa kaunti wanajivinjari. 

MCA wa Karen David Mberia alisema MCAs wanapaswa kutumia njia na kamati zinazofaa kama vile Kamati ya Madaraka na Mapendeleo kuelezea wasiwasi wao.